Mtibwa Sugar waifuata Singida Utd
Kikosi cha soka cha Mtibwa Sugar kimeondoka Jumatano asubuhi ya April 4, 2018 kuelekea mkoani Singida kucheza mchezo wa ligi raundi ya 23 dhidi ya Singida United mchezo utakaofanyika Ijumaa ya April 6 katika uwanja wa Namfua mjini humo.
Akizungumza na mtandao huu wakati wa kuanza kwa safari hiyo Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar Zuberi Katwila amesema watakuwa na ratiba ngumu, kwani baada ya kucheza na Singida itawabidi kurudi Morogoro kucheza na Simba SC hivyo wanajipanga kwa ugumu wowote ambao upo mbele yao.
"Baada ya mazoezi ya takribani siku mbili toka mchezo wetu na Azam wa kombe la FA, sasa tunaelekea Singida kucheza dhidi ya Singida United, tumeshajiandaa na ugumu wa ratiba uliopo mbele yetu kwani tayari ishapangwa hatuwezi kuipangua, na tunaweza kupata matokeo licha ugumu huo, na tutapata matokeo," Katwila amesema.
Mtibwa Sugar inauendea mchezo wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwatoa Azam katika kombe la Shirikisho wakati pia wapinzani wao Singida United wakitoka kuwatoa Yanga katika michuano hiyo hiyo maarufu kama Azam Sports Federation Cup.
Aidha katika michezo ya hivi karibuni Mtibwa Sugar wamekuwa hawana matokeo mazuri kwani katika michezo mitano ya mzunguko wa pili wameshindwa kupata ushindi wowote wakifungwa michezo minne na kutoka sare mchezo mmoja.
Mtibwa wana alama 27 wakiwa katika nafasi ya 6 huku tayari wakiwa wamecheza michezo 20 msimu huu wakati wapinzani wao Singida United wakiwa katika nafasi ya tano na alama zao 36.
Join us on WHATSAPP
Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.