Kongo "watoto" wawasili nchini kuivaa Ngorongoro
KIKOSI cha timu ya soka ya vijana ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kimewasili nchini juzi usiku tayari kwa mechi yao ya kwanza dhidi ya wenzao wa Tanzania (Ngorongoro Heroes) itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hizo zinakutana kuwania tiketi ya kucheza fainali zijazo za vijana za Afrika (AFCON U-20) zitakazofanyika mwakani huko Niger.
Akizungumza jana jijini, Kaimu Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yako katika hatua za mwisho na kiingilio cha chini kimepangwa kuwa ni Sh. 1,000 huku cha juu kikiwa ni Sh. 3,000 kwa viti vya VIP A, B na C.
"Sasa tuko katika maandalizi ya mechi yetu ya vijana na wapinzani wao DRC wamewasili nchini jana (juzi) usiku na kesho (leo) wataanza kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa," alisema Ndimbo.
Aliongeza kuwa wanatarajia mechi hiyo kuwa na ushindani kutokana na ubora wa timu zote mbili, lakini wageni wakitaka kulipiza kisasi baada ya kaka zao kufungwa mabao 2-0 na Taifa Stars mapema wiki hii.
Katika kujiandaa na mchezo huo, Ngorongoro Heroes inayonolewa na Kocha Mkuu, Ammy Ninje, ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Morocco ambapo ilishinda bao 1-0 na baadaye kuifunga Msumbiji magoli 2-1.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.