Yanga wapata ahueni
Mabingwa wa Tanzania Bara timu ya soka ya Dar Young Africans inatarajiwa kuwakosa wachezaji watatu kuelekea mechi ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana.
Kadhalika Yanga watapata ahueni baada ya wachezaji wao wanne ambao walikosa michezo kadhaa kutokana na matatizo mbalimbali kurejea kikosini na wanatarajiwa kucheza katika mchezo huo utakaopigwa leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wachezaji ambao watakosa licha ya kurejea kwenye mazoezi ni pamoja na Donald Ngoma, Amiss Tambwe na Vincent Andrew ambao wao wanaweza kucheza kwenye mechi ya marudiano.
Thaban Kamusoko, Yohana Mkomola, Juma Mahadhi, Nadir Haroub Canavaro, Abdallah Shaibu Ninja na Obrey Chirwa wao tayari wamesharejea na wanatarajiwa kuwa sehemu ya mchezo huo.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo Charles Boniface Mkwasa amewaomba wachezaji wote ambao watapewa majukumu ya uwanjani kuhakikisha wanawajibika ili kuweza kupata matokeo mazuri yatakayowafanya kusonga mbele katika hatua inayofuata.
"Sisi tunania ya dhati kabisa ya kufanya vizuri na tumeshajipanga lakini pia itategemea na jitihada zetu sisi uongozi na jitihada za wachezaji,".
"Ninawaomba wachezaji wawe makini tutumie vizuri mechi ya nyumbani, tupate matokeo mazuri ili iwe njia rahisi ya kusonga mbele tukifuatilia mechi ya marudiano," Mkwasa amesema
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.