Yanga Kwenda Kenya Siku Hii Hapa.


Msimu wa ligi Kuu ya Vodacom 2017-18 umemalizika kwa machungu makubwa kwa mashabiki wa Yanga baada ya kuishuhudia timu yao ikilazwa mabao 3-1 na Azam FC.

Baada ya kumalizika ligi, keshokutwa Alhamisi Yanga inatarajiwa kwenda nchini Kenya kushiriki michuano ya SportPesa Super Cup, michuano ambayo ni lazima kushiriki kwa timu zinazodhaminiwa na SportPesa.

Ratiba ya michuano hiyo inayoanza Juni 03 imetolewa jana ambapo saa saba kamili mchana wa siku hiyo, Yanga itachuana na KK HomeBoyz kwenye mchezo wa ufunguzi.

Baadae siku hiyo hiyo Gor Mahia itachuana na JKU mchezo ukitarajiwa kuanza saa tisa na robo wakati Simba, mabingwa wa VPL msimu huu wao watacheza Juni 04 dhidi ya K Sharks saa tisa kamili Alasiri.

Singida United ambayo Juni 02 inakabiliwa na mchezo wa fainali ya kombe la FA dhidi ya Mtibwa Sugar, itashuka dimbani Juni 05 kucheza na AFC Leopards mchezo ukitarajiwa kuanza saa tisa Alasiri.

Michuano hiyo ni ya mtoano, timu nne zitakazoshinda michezo ya kwanza zitatinga hatua ya nusu fainali.

Michezo ya nusu fainali itapigwa Juni 07 wakati ile ya fainali na mshindi wa tatu na nne itapigwa Juni 10.

Bingwa wa michuano hiyo atanyakua karibu Mil 68 pamoja na kupata nafasi ya kusafiri kwenda nchini Uingereza kucheza na Everton katika dimba la Goodison Park

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.