Ngassa Kurejea Yanga, Sanga Afunguka Haya..


KAIMU Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, amefunguka kuwa hatima ya kurejea Jangwani kwa mshambuliaji wao wa zamani, Mrisho Ngassa anayekipiga Ndanda FC, ipo mikononi mwa kocha wao, Mwinyi Zahera na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika.

Ngassa amekuwa akihusishwa kutaka kurudi Jangwani kutokana na kiwango alichokionyesha msimu huu, lakini pia mapenzi ya dhati aliyonayo kwa timu yake hiyo.

Ikumbukwe kuwa kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Ndanda uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara, Ngassa alionyesha kiwango cha hali ya juu.

Licha ya Yanga kushinda mabao 2-1, Ngassa aliiongoza vyema timu yake ikiwamo kuchangia kwa kiasi kikubwa bao la kufutia machozi.

Akizungumza na BINGWA jijini Dar es Salaam juzi, Sanga alisema ameshangazwa na maneno yanayoenezwa na mashabiki na wanachama wa timu hiyo kwamba hamtaki nyota huyo kikosini, jambo ambalo si kweli.

“Nimesikia maneno mengi sana kuhusu suala la Ngassa, hata siku moja siwezi kuiingilia Kamati ya Usajili, nafikiri Nyika na kocha  Zahera wana nafasi kubwa safari hii kuamua juu ya hatima ya Ngassa,” alisema Sanga.

Alisema upande wake, hana tatizo na mshambuliaji huyo kurejea Jangwani kwani anatambua uwezo wake na mapenzi ya dhati aliyonayo kwa timu hiyo.

“Sina tatizo hata kidogo, Ngassa ruksa kurudi Yanga, lakini kama Kamati ya Usajili na kocha watamkubali. Lazima wanachama waelewe hilo, milango iko wazi kabisa,” alisema Sanga.

Wakati huo huo, Sanga alisema wanatarajia kufanya kikao kizito kujadili mambo mbalimbali yanayohusu klabu yao, lakini ajenda kubwa ikiwa ni usajili na ushiriki wao katika michuano ya SportPesa na Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

“Mambo tutakayoyajadili ni usajili, kuangalia ni namna gani tunaweza kufanya usajili wa nguvu na wenye tija. Lakini pia, tutajadili masuala mengi kwa faida ya klabu,” alisema Sanga.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.