Kikosi bora cha mwaka ligi kuu ya Tanzania Bara hiki hapa Okwi ndani Bocco nje

Kikosi bora cha mwaka ligi kuu ya Tanzania Bara hiki hapa Okwi ndani Bocco nje
Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaelekea ukingoni, huku kukiwa na mabadiliko makubwa kwa timu pamoja na wachezaji wakionesha kiwango cha hali ya juu uwanjani.


John Bocco na Marcel Kaheza wakiwa ni wachezaji wazawa pekee waliofunga magoli zaidi ya kumi.

Azania post inakuletea kikosi cha mwaka msimu huu haswa kwa kuangalia mchezaji amesaidiaje timu yake. Mfumo ukiwa 4:4:2.

Aishi Manula

Wengi wanaamini huyu ndiye kipa namba moja Tanzania 'Tanzania one' hasa kutokana na umahiri wake wa kuokoa michomo mbalimbali uwanjani.

Ana 'clean sheets' 18 idadi ambayo haijafikiwa na kipa mwingine yeyote katika msimu wa ligi wa 2017/2018, hivyo msimu huu anastahili kukaa langoni kikosi cha mwaka.

Hassan Kessy

Bila ya ubishi kwa nafasi yake, wengi wamecheza vizuri lakini yeye amesababisha kupatikana kwa alama 9 kwa msimu huu kwa pasi za mwisho pamoja na kuchangia kwa kufunga magoli yeye mwenyewe.

Asante Kwasi

Beki huyu raia wa Ghana amefanya vizuri sana msimu huu. Amekuwa akicheza kama beki wa kati kama wakati timu yake ya Simba ilipokutana na Lipuli FC. Ni katika dirisha dogo la usajili ndipo mnyama Simba ilifanikiwa kunasa saini ya mchezaji huyu, na kusaidia kupiga mabao 7 ikiwa mawili yakipatikana akiwa na Simba na matano Lipuli. Huyu ana uwezo wa kucheza mfumo wowote uwanjani.

Erasto Nyoni

Kwa msimu huu hakuna beki aliyenyumbulika zaidi yake yeye, kila anapozidi kuwa na umri mkubwa ndo anakuwa mtamu, atakumbukwa kwa kuiua Yanga April 29 mwaka huu.

Kelvin Yondani

Licha ya ujeuri alionao bado beki bora sana Tanzania, yeye akisimama na Nyoni mambo yanakuwa moto.

Jonas Mkude

Alibaniwa nafasi wakaki wa kocha Omog lakini alipopata nafasi kila mmoja aliona kazi yake.

Tafadzwa Kutinyu

Huyu jamaa anatoka Singida United, ameiua Yanga kombe la FA lakini pia bado anafanya vizuri katika timu yake.

Shiza Kichuya

Mkuu wa idara ya pasi za mwisho, licha ya umbo lake dogo bado amefanya vizuri sana.

Emanuel Okwi

Hakuna haja ya kumuelezea sana amepiga magoli 20 na kuwa mwiba.

Marcel Kaheza

Amepiga magoli 13 huyu anacheza Majimaji akitokea klabu ya Simba. Hapa kutakuwa na mjadala mkubwa juu ya kumuacha Bocco licha ya kazi nzuri aliyofanya, Kaheza amechukua nafasi yake kwa timu aliyonayo na kuweza kutundika magoli 13 Bocco amezungukwa na watu wengi wanaoweza kumlisha.

Je wewe kikosi chako kipi unaweza kupitia ukurasa watu wa Facebook, Instagram na Twiter kutoa maoni yako.

Source:Azania Post

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.