JKT Tanzania Waitahadhalisha Singida United Nusu Fainali ASFC


Uongozi wa klabu ya soka ya JKT Tanzania umesema tayari umeshawajua wapinzani wao katika hatua ya nusu fainali ya Azam Sports Federations na watakwenda kujipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi na kutinga fainali.

JKT Tanzania ambao waliwatoa Tanzania Prisons kwa kuwachapa mabao 2-0 hapo Jumamosi wamesafiri kutoka mkoani Mbeya na kwenda kuangali mchezo wa Singida United na Yanga kwa lengo la kujua watapambana vipi na Yule watakayekutana naye hatua ya nusu fainali.

Akizungumza na mtandao huu, kocha wa JKT Tanzania Bakari Shime amesema maamuzi ya kuja kuangalia mchezo huo ambao Singida United ndio walioibuka na ushindi umewasaidia kwani sasa wanajua aina ya uchezaji wa Singida pamoja na uchezaji wa mtu mmoja mmoja.

“Kuja hapa ni kuangalia robo fainali hii, kujua mtu mmoja mmoja na mipango yao kama timu ipoje na kwa namna gani tutacheza nao, Kwa vyovyote vile tumepata kuona, approach ya Singida vile wapo, tumepata faida kubwa kuja kuona mchezo huu” amesema Shime.

Aidha kwa upande wa mwenyekiti wa klabu hiyo Kanali Hassan Mabena ametanabaisha kuwa nidhamu na utulivu wa wachezaji na benchi la ufundi ndio umesaidia wao kufikia hatua hiyo.

“Tumekuwa na nidhamu kubwa, na utulivu wa hali ya juu na ndio maana tumefika hatua hii, najua ugumu wa hatua tuliyofikia, timu zote tunaziheshimu hata Singida tunawaheshimu, tumekuja Singida kuangalia namna gani tunawakabili, lengo letu ni kutwaa ubingwa katika michuano hii,” amesema.

JKT Tanzania imepangwa kucheza na Singida United katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, huku nusu fainali nyingine itawakutanisha Mtibwa Sugar na Stand United ya kutoka mkoani Shinyanga.

Ikumbukwe bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi katika michuano ya kombe la Shirikisho inayosimamiwa na Shirikisho la soka barani Afrika (CAF).
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.