Township Rollers Waitandika Yanga Waiachia Mlima Mzito



Mabingwa wa soka Tanzania Bara Dar Young Africans wameanza vibaya raundi ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa mabingwa wa Botswana Township Rollers ‘POPA POPA EA IPOPA’.

Yanga wakicheza chini ya kiwango muda mrefu wa mchezo huo wakiwaacha Rollers ambao ndio wageni kuonekana kama wenyeji wa mchezo wakicheza kandanda safi na la kuvutia kwa muda wote wa mchezo.



Mechi ilianza kwa kasi kwa kila timu kujaribu kutafuta bao la mapema, kwani katika dakika tano tu za mwanzo zilionesha wazi ni nini kila timu ilikuwa inahitaji katika mchezo huo.

Ndani ya dakika hizo tayari nafasi za wazi tatu, mbili za Township Rollers moja ikiwa ya Joel Mogorosi ambaye alikosa umakini alipokuwa katika eneo la 18 la Yanga, pamoja na kutoweza kutumia makosa ya kipa Ramadhan Kabwil katika dakika ya nne baada ya kurudishiwa mpira na kushindwa kuuondosha kwa haraka.

Bao la Rollers

Iliwachukua dakika 10 tu Rollers kuandika bao baada ya kiungo Lemponye Tshireletso kupiga shuti la takribani umbali wa mita 25 ambalo lilikwenda moja kwa moja na kumshinda kipa Ramadhan Kabwili.

Baada ya bao hilo Township Rollers hawakutulia kwani waliendelea kulishambulia lango la Yanga kama nyuki na dakika ya 13 almanusura waandike bao la pili lakini mlinzi Said Juma Kamapu alikaa vyema na kuondosha mpira na kuwa kona butu.

Yanga waliendelea kufanya makosa katika eneo lao la ulinzi na kuwaruhusu Rollers kuendelea kutia pressure ambapo bila umakini walirudishiana mpira kipa wao lakini Lemponye aliuwahi na wakati akijaribu kumtia chenga Kabwili alishindwa na kuutoa mpira nje.

Katika dakika ya 18 Yanga nao walijaribu kulitia kashikashi lango la Rollers lakini shuti la Pappy Kabamba Tshishimbi alilopiga baada ya kupokea pasi ya Hassan Kessy lilipaa na kuwa goal kick.

Yanga walitulia licha ya washambuliaji wa Rollers Joel Mogorosi na Motsholetsi Sikele kuendelea kuisumbua ngome yao.

Bao la Chirwa

Dakika ya 29 Yanga wakigongeana kwa umakini mkubwa, mpira ukianzia kwa Piusi Buswita na baadae ya Pappy Kabamba ulimkuta Obrey Chirwa ambaye alikutana na kipa Keagile Kgosipula na kuchagua sehemu ya kupiga na kuandika bao la kusawazisha.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote zilitoka zikiwa sawa licha ya Township Rollers kuonekana kuongoza katika umiliki wa mpira kwa asilia 51 dhidi ya 49 za wenyeji Yanga.

Kipindi cha pili Yanga walianza vizuri tofauti na walivyoanza katika dakika 25 za kipindi cha kwanza, wakicheza kwa kuonana na kupiga mashuti ya mbali ambayo mengi yalikuwa yakitoka nje bila hata kulenga lango.

Yanga walikuwa kama wanabahati hivi katika dakika ya 60 pale ambapo Ivan Ntege alipoambaa na mpira na kutoa pasi murua ambayo kama Lemponye Tshireletso angekuwa makini na kichwa alichopiga basi angeiandikia Rollers bao la pili.

Yanga walijibu kwa shambulizi la Ibrahi Ajiba ambaye alimwaga krosi kwa Obrey Chirwa katika dakika ya 62 lakini krosi yake ilikuwa kubwa na kutoka nje na kuwa goal kick, hata hivyo dakika moja baadae Pius Buswita alipata nafasi ya kupiga shuti lakini kwa mara nyingine shuti lake likaota mbawa.



Kocha Goerge Lwandamina ilimlazimu kufanya mabadiliko kwa kumtoa Emmanuel Martin na kumuingiza Geofrey Mwashiuya ili kufufua eneo la mashambulizi, lakini pia Juma Mahadhi akaingia nafasi ya Ibrahim Ajib.



Yanga wakiwa na hamu ya kupata bao la pili, Township Rollers walifanya shambulizo la kushtukiza kutoka kwa Segolame Boy ambaye alitoa pasi ndefu iliyomfikia Joel Mogorosi ambaye naye bila kutuliza akampasia Motsholetsi Sikele ambaye alifunga bao la pili.



Hadi kipyenga cha mwisho cha mwamuzi Pacifique Ndabihawenimana kutoka Burundi kinapulizwa Yanga walitoka kichwa chini kwa mabao 2-1 na kuwafanya kuwa na mlima mrefu pale watakaporudiana baadae mjini Gaborone.

Yanga watahitaji ushindi wa maba 2-0 au zaidi ili kufuzu hatua ya makundi ya klabu bingwa Afrika ili kujiwekea rekodi ya toka mwaka 1989 walipofuzu kwa mara ya kwanza na ya mwisho katika hatua ya makundi.

Vikosi vilivyocheza.

Yanga SC: Ramadhan Kabwili, Gadiel Michael Mbaga, Juma Said Makapu, Kelvin Yondan, Ramadhan Hamis Kessy, Patto Ngonyani, Pappy Kabamba Tshishimbi, Ibrahim Ajib Migomba, Pius Buswita, Emmanuel Martin na Obrey Chirwa.

Akiba: Youthe Rostand, Juma Abdul, Mwinyi Haji Mngwali, Raphael Daud, Yussuf Mhilu, Juma Mahadhi na Geofrey Mwashiuya.

Township Rollers: Keeagile Kgosipula (GK), Tshepo Motlhabankwe, Simisani Mathumo, Mosha Gaolaolwe, Kaone Vanderwesthuizen, Motsholetsi Sikele, Maano Ditshupo (C), Lemponye Tshireletso, Segolame Boy, Mthokozisi Msomi na Joel Mogorosi

Akiba: Tshepo Matete, Ivan Ntege, Edwin Olerile, Gape Mohutsiwa, Oscar Ncenga, Thato Bolweleng na Mwampule Masule (GK)

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.