Simba wagoma kumuuza Okwi kwa Waarabu
UONGOZI wa Simba, umedai kuwa hauwezi kumuuza mchezaji wao Mganda, Emmanuel Okwi kwa timu ya Al Masry na umesisitiza kuwa sasa wanawaza kuhusu ubingwa na siyo kuuza wachezaji.
Okwi ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea timu ya Sports Club Villa ya kwao Uganda kwa ada ya shilingi milioni 115, ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara akiwa nayo 16 akifuatiwa na Obrey Chirwa mwenye 12.
Katika mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, ilielezwa kuwa Waarabu walivutiwa na ‘udambwiudambwi’ wa Mganda huyo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Simba, Said Tully, alisema kuwa kwa sasa wanachoweza kuwaza ni kuhusu mechi zao kumi zilizobakia kwenye ligi kuu, masuala ya kuuza wachezaji bado muda wake, ila kuhusu taarifa za kutakiwa na Al Masry hawajaweza kuzungumza nao suala hilo.
“Tumebakiwa na mechi kumi hivyo mipango yetu na mikakati yetu ni kuhakikisha tunashinda mechi zote na kuweza kuchukua ubingwa lakini pamoja na ushindani wa kwenye ligi tunajua kuwa kuna makosa nyuma timu imefanya na kuweza kushindwa kupata pointi lakini sisi kama uongozi tumejipanga kuhakikisha kuwa makosa hayo hayajirudii na hakuna njia nyingine zaidi ya kufanya maandalizi ya kutosha na kuweza kushinda mechi zote.
“Hakuna maongezi yoyote tuliyofanya na Al Masry kuhusu kumuuza Okwi na huu siyo muda wa kuuza wachezaji na agenda yetu namba moja sasa hivi ni kushinda ligi na kuchukua ubingwa na hatuwezi kuzungumza masuala yoyote, hivyo tutazungumza hilo msimu ukiwa ushamalizika, sasa hivi agenda yetu ni kupambana kama tukiweza kuchukua ubingwa au tukishindwa ndiyo tutajua nani tumuuze nani tubaki naye,” alisema.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.