Mwamuzi Aliyetuhumiwa Kupanga Matokeo Klabu Bingwa Asimamishwa Zanzibar..
Chama cha soka Visiwani Zanzibar (ZFA), kimemsimamisha mwamuzi Mfaume Ali Nassoro ili kupisha uchunguzi wa shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kuhusu tuhuma za upangaji wa matokeo zinazowakabili waamuzi wanne wa Tanzania akiwemo mwamuzi huyo.
Akizungumza na mtandao huu, afisa habari wa chama hicho, Ali Bakari ‘Cheupe’ amesema wamefikia maamuzi hayo ili kuweza kuwapa nafasi nzuri CAF kuendelea kufanya uchunguzi wao bila ya kupingamizi chochote.
“Tumeshamuandikia barua (Mfaume) kuwa tumemsimamisha kwa muda hadi pale CAF itakapokamilisha uchunguzi wake dhidi ya waamuzi hao wanne, kwa hiyo mara baada ya kukabidhiwa barua yake hatoruhisiwa kuchezesha mchezo wowote hapa Zanzibar,” Bakari amesema.
Katika kuleweka sawa hilo, Bakari amesema hawajamuhukumu mapema mwamuzi huyo bali kitu ambacho wamekifanya ni cha kiuweledi ili kuweza kupisha uchunguzi wa jambo hilo kuwa huru na pindi CAF watakapokamilisha uchunguzi wao basi watajua cha kufanya.
“Kwetu sisi hatuoni kama tumetoa maamuzi ya mapema au kumuhukumu kabla ya ukweli kupatikana na wala hatufurahii kwa hili linalomkuta, kwani huyu sasa ni mwamuzi ambaye anatuhumiwa, kwa hiyo hawezi kuchunguzwa wakati bado anachezesha ni vizuri akawa nje ya mambo hayo kwanza,” Bakari Cheupe amesema.
Waamuzi wanne
Ikumbukwe kuwa Mfaume pamoja na waamuzi wengine watatu wa Tanzania Frank John Komba Soud Idd Lila na Israel Omusingi Njunwa Mujuni walifunguliwa mashtaka na CAF kwa tuhuma za upangaji wa matokeo katika mchezo wa klabu bingwa Afrika kati ya Lydia Ludic Burundi Academic ya Burundi na Rayon Sports ya Rwanda.
Inasadikika kuwa kuwa viongozi wa Rayon Sports ya Rwanda walikutwa kwenye chumba cha mmoja wa waamuzi wa Tanzania siku moja kabla ya mchezo huo ambao ulifanyika nchini Burundi na kuzuka vurugu kubwa, kitendo ambacho kililipotiwa na kamishna wa mchezo huo Gladmore Muzambi na CAF kuona umuhimu wa kufungua uchunguzi kuhusiana na sakata hilo.
Aidha katika mchezo huo ambao ulifanyika nchini Burundi, Rayon Sports waliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kufanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1.
Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.