Wajue Zaidi Wapinzani Wa Yanga 'Township Rollers Fc"..
Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, itaumana na mabingwa wa Botswana, Township Rollers kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kuwaondoa El Merreikh ya Sudan.
Yanga wametinga hatua hiyo baada ya kuifunga St. Louis ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 2-1, itacheza mchezo wake wa kwanza nyumbani kwenye uwanja wa Taifa Machi 6 au 7 kabla ya kurudiana ugenini wiki moja baadaye.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara watapaswa kujipanga vyema kuwakabili Wabotswana ambao wanaonekana wako imara wakicheza mfumo wa 4-5-1 unaopendwa kutumiwa na kocha wa timu hiyo, Nikola Kavazovic.
Kocha huyo anapenda kutumia mfumo huo hasa anapocheza ugenini huku kwenye safu yake ya ushambuliaji akimtegemea straika, Joel Mogorosi, ambaye alifunga bao kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya El Merreikh ambao ulimalizika kwa kufungwa magoli 2-1.
Township Rollers ambao wanaongoza katika Ligi Kuu ya Botswana kwa tofauti ya pointi tisa dhidi ya Miscellaneous inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 34, ni wazuri katika mashambulizi ya kushtukiza jambo ambalo Yanga watatakiwa kuwa makini kwenye mchezo huo.
Kikosi cha Yanga kilichoko chini ya kocha George Lwandamina kimerejea nchini jana usiku kikitokea Shelisheli tayari kuanza maandalizi ya kuwakabili wageni hao na vile vile kuendelea na mbio za kutetea ubingwa wa ligi wanaoushikilia.
Hata hivyo kabla ya mchezo huo wa kimataifa, Yanga itacheza michezo mingine mitatu, mchezo wa kwanza wa mashindano ya Kombe la FA utakaofanyika Jumapili mjini Songea, Ruvuma dhidi ya Majimaji.
Baada ya mchezo huo, Yanga itaendelea kuwa ugenini kwa kuwafuata Ndanda FC mkoani Mtwara kisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.