Djuma Awapuuza Waarabu .

Kikosi cha wekundu wa Msimbazi, timu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam imerejea kwa mafungu alfajiri ya kuamkia Februari 22 mwaka huu wakitokea nchini Djibouti walipokuwa na mchezo wa kuwania taji la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendarmarie Tnale.
Akizungumza na mtandao huu mara baada ya kuwasili nchini kocha msaidizi wa Simba Masoud Djuma Irambona amesema mchezo wao ulikuwa mgumu na wanafurahi kuona wamefuzu hatua ya kwanza ya michuano hiyo ambayo ni ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya vilabu Afrika.
Aidha Djuma amesema baada ya kurejea nchini mawazo yao sasa wanaelekeza katika maandalizi ya mchezo wa ligi dhidi ya Mbao FC utakaofanyika Jumatatu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Alipoulizwa kuhusu maandalizi ya mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Al Masry yataanza lini, Djuma alidadavua kuwa kwa sasa nguvu zao kwanza wanazielekeza kwenye mchezo dhidi ya Mbao na si vinginevyo.
“Kwanza hatuwaangalii timu ya Al Masry kama wengi wanavyodhani, mchezo uliopo mbele yetu ni mchezo wa ligi dhidi ya Mbao, ligi ni zaidi kuliko Al Masry, kwanza mechi yenyewe ipo mbali, itakuja siku yake tutaiandaa,” amesema.
Kipigo cha 5-0
Walipokuwa nchini Djibouti, mabingwa hao wa kombe la Shirikisho Tanzania Bara walifanikiwa kuichapa Gendarmarie kwa bao 1-0 na hivyo kuwatoa kwa jumla ya mabao 5-0 baada ya mchezo wa awali kushinda kwa mabao 4-0.
Simba watakutana na Al Masry Machi 9 mwaka huu katika mchezo wa kwanza wa kombe la Shirikisho utakaofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar, kabla ya kurudiana Machi 16 mjini Ismailia katika uwanja wa Ismaïlia unaoweza kubeba mashabiki elfu 15.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.