YANGA YAMSHUSHA MRITHI WA NGOMA
Kikosi cha Yanga kimemshusha straika wa nguvu, Mnigeria Ogochukwu James kutoka Manzini Wanderers ya Swaziland kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mzimbabwe Donald Ngoma aliyemalizana na timu hiyo.
Ngoma ameondolewa kwenye mipango ya Kocha Mkongo, Mwinyi Zahera na mabosi wa klabu hiyo wakafanya mipango ya haraka kumnasa mshambuliaji huyo ambaye ameshaanza majaribio ndani ya kikosi hicho.
Straika huyo mpya mtihani wake mkubwa ni mara Kocha Zahera atakaporudi kutoka DR Congo kwani sasa anafanya majaribio hayo chini ya makocha wasaidizi akiwemo, Shadrack Nsajigwa.
Mwanaspoti iliyokuwa inajua ujio wa Mnigeria huyo mwingine mbali na Kola, ambaye anacheza soka la kulipwa Swaziland katika klabu ya Manzini Wanderers na jana Jumatatu ilimfumania Makao Makuu ya Yanga wakati akijiandaa kwenda mazoezini.
"Huyu jamaa amekuja kwa ajili ya kujaribiwa na kama ataliridhisha benchi la ufundi atasajiliwa kwa sababu Yanga tunataka tufanye vizuri baada ya msimu huu kuyumba kidogo," amesema mmoja wa vigogo wa Yanga aliyeombwa kuhifadhiwa jina lake.
Hata hivyo Mwanaspoti linafahamu, James na Kola aliyepo kwenye mipango ya Yanga sambamba na washambuliaji wengine wawili wazawa wanawindwa ili kuchukua nafasi ya Ngoma aliyevunjiwa mkataba wake kutokana na kuwa majeruhi wa muda mrefu.
Katika hatua nyingine, kiungo Papy Kabamba Tshishimbi amerudi nchini kutoka Kongo na leo atafanya mazoezi na wenzake, huku Pius Buswita, Abdallah Shaibu 'Ninja' na Gadiel Michael waliokuwa majeruhi na kukosa mechi zilizopita wamepona, huku Andrew Vincent Dante akiukosa mchezo wa leo dhidi ya Mbao kwa kuwa na kadi tatu za njano.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.