Yanga Kuwafuata Mbeya City Leo
Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuondoka leo kwa usafiri wa Ndege kwenda mkoani Mbeya tayari kwa mchezo wa ligi kuu ya Vodacom dhidi ya Mbeya City utakaopigwa kwenye dimba la Sokoine kesho Jumapili, April 22 2018.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na uongozi wa Yanga jana, Yanga itasafiri bila kiungo wake Papi Tshishimbi aliyepata majeraha kwenye mguu wake wa kulia katika mchezo dhidi ya Wolaitta Dicha.
Tshishimbi anabaki jijini Dar es salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Hata hivyo wachezaji Ibrahim Ajib (alikuwa mgonjwa) na Andrew Vicent aliyekuwa majeruhi wote wamerejea kikosini tayari kwa mchezo huo.
Yanga pia itawakosa Maka Edward, Ramadhani Kabwili na Said Mussa ambao wamesafiri na kikosi cha Ngorongoro Heroes kuifuata DRC kwa ajili ya mchezo wa marudiano kusaka tiketi ya michuano ya vijana ya AFCON U20.
Yanga iko nyuma kwa tofauti ya alama 11 dhidi ya Simba ambayo leo inashuka kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa kuikabili Lipuli FC.
Ni matokeo pekee ya ushindi yatakayoweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wa VPL msimu huu.
Baada ya mchezo huo, mchezo unaofuata ni dhidi ya Simba uwanja wa taifa, Jumapili ijayo, April 29.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.