Yanga Mmeipata Hii Ya Kocha Wa Township Rollers?
Kocha mkuu wa kikosi cha Township Rollers Mserbia Nivola Kavazovic amesema wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo wao wa raundi ya kwanza ya klabu bingwa Afrika dhidi ya mabingwa wa Tanzania Dar Young Africans.
Kavazovic amesema katika kujiandaa huko tayari wameshaangalia mechi nne walizocheza Yanga hivi karibuni ambapo katika kuziangalia tayari wameshatambua udhaifu wao pamoja na nguvu yao.
“Tumeziangalia na kuzichambua mechi takribani nne ambazo Yanga wameshacheza, mbili za nyumbani na mechi mbili za ugenini tumegundua kitu, lakini siwezi kuwaambia ni mambo ya kiufundi kidogo,” amesema.
Tutashambulia
“Ukiniuliza kuhusu mbinu nitakazotumia kuwazuia Yanga sitakuambia, lakini ninakuambia tutakwenda kusukuma mashambulizi ili kuwalazimsha wafanye makosa yao na kuwazuia sehemu wanalipo imara,” Kavazovic amesema.
Kocha huyo amesema hali ya hewa ya sasa ya jiji la Dar es Salaam ni nzuri ukilinganisha na hali waliyoikuta walipokuwa nchini Sudan na hilo linazidi kuwapa matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo.
Township Rollers watakwaana na Yanga katika mchezo ambao utafanyika Jumanne ya Machi 6 katika uwanja wa Taifa, kuanzia majira ya saa 10:00 jioni.
Tayari waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Burundi wameshawasili ambapo mwamuzi wa kati atakuwa Pacifique Ndabihawenimana akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Willy Habimana na mwamuzi msaidizi namba mbili Pascal Ndimunzigo wakati Kamishna wa mchezo huo anatoka Swaziland ambaye ni Mangaluso Jabulani Langwenya.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.