Watano Azam Fc Waitwa Ngorongoro Heroes
WACHEZAJI watano wa timu ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20, wameitwa kujiunga na timu ya Taifa ya Tanzania ya umri huo ‘Ngorongoro Heroes’.
Nyota walioula kutoka Azam FC ni beki wa kati Oscar Masai, beki wa kushoto, Said Issa, viungo ni Mohammed Mussa ‘Kijiko’, Rajab Odasi na mshambuliaji Paul Peter, huku Ibrahim Ally, aliyekuwa awali ameitwa akienguliwa kutokana na majeraha ya misuli ya paja.
Heroes inayofundishwa na Kocha Oscar Milambo, chini ya Mkuu wa Soka la Vijana wa TFF, Kim Poulsen, inajiandaa na mechi za kufuzu mataifa ya Afrika (U-20 Afcon Qualifier) fainali zitakazofanyika nchini Nigeria mwakani.
Timu hiyo imepangwa kuanza na DR Congo kwenye mchezo wa raundi ya kwanza utakaofanyika Machi 30 mwaka huu jijini Dar es Salaam huku ule wa marudiano ukipigwa Aprili 22 mwaka huu, jijini Kinshasa, Congo na mshindi wa jumla wa mchezo huo atakata tiketi ya kucheza na Mali anayeanzia raundi ya pili.
Kwa mujibu wa barua pepe iliyotumwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, kuja Azam FC, imeeleza kuwa wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini kesho Jumanne saa 10.00 jioni katika Hosteli za TFF, zilizopo Karume jijini Dar es Salaam.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.