Simba Kuweka Kambi Cairo


Wekundu wa Msimbazi, Simba wataondoka nchini kesho kuelekea Cairo, Misri ambapo wataweka kambi ya muda kabla ya kuwafuata wenyeji wao, Al Masry.

Al Masry inatarajia kuikaribisha Simba Jumamosi katika mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Machi 7 kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara amesema kuwa kikosi cha timu hiyo kitaondoka nchini kesho na kitaweka kambi ya muda jijini Cairo na siku inayofuata itaanza safari kuelekea Port Said.

Manara amesema kuwa maandalizi ya safari yameshakamilika na kinachosubiriwa ni Kocha Mfaransa, Pierre Lechantre, kutoa orodha ya mwisho ya wachezaji watakaosafiri.

"Idadi ya wachezaji itaamuliwa na kocha, yeye ndiye anayejua askari ambao watamfaa kwenye vita hii tunayokwenda kuikabili, kwa upande wa viongozi, kila kitu kinakwenda vyema, sisi ndio wazoefu wa mashindano ya kimataifa," alisema Manara.

Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.