AZAM: Hatuhitaji kufanya makosa yoyote vs KMC


KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa timu hiyo haitakiwi kufanya makosa yoyote kuelekea mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya KMC utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kupata sare mbili mfululizo katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Kagera Sugar (1-1) na Lipuli (0-0) kabla ya hapo ikitoka kupoteza bao 1-0 dhidi ya Simba.

Cioaba amesema kuwa mchezo huo ni muhimu sana na anawaamini wachezaji wake watafanya kweli kwa kuibuka na ushindi.

“Wachezaji wanafahamu michuano hii kuwa ni migumu kama huweki umakini wa kushinda mchezo basi utapata tatizo kwa kuwa ni mchezo mmoja tu na sio kama ligi, nataka kila mmoja afahamu hali hii na kuonyesha umakini kwenye mchezo huu.

“Nawajua wapinzani wetu kuwa ni timu nzuri, wachezaji wanatakiwa kumuheshimu mpinzani na kuingia Jumamosi uwanjani na kucheza kwa nguvu na kushinda mchezo,” alisema.

Timu hizo zinakutaka kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo, lakini ziliwahi kucheza mchezo wa kirafiki Agosti mwaka jana wakati wa maandalizi ya msimu na Azam FC kushinda bao 1-0, lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Nahodha Msaidizi Agrey Moris baada ya Wazir Junior kuangushwa katika eneo la hatari.

Azam FC imefika hatua hiyo baada ya kuinyuka Shupavu mabao 5-0 kwenye mchezo ambao ilishuhudiwa mshambuliaji kinda Paul Peter, akipiga ‘hat-trick’, mengine yakifungwa na Yahya Zayd na Idd Kipagwile.

KMC iliyopanda Ligi Kuu kuelekea msimu ujao, iliichapa Toto Africans ya Mwanza mabao 7-0.

Tayari kikosi cha Azam FC kimeshaanza maandalizi ya kwanza jana jioni kuelekea mchezo huo, ambapo wachezaji pekee waliokosekana ni Nahodha Himid Mao ‘Ninja’ na mshambuliaji Wazir Junior, waliokuwa majeruhi.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.