SIMBA YAIFUATA MAJIMAJI BILA BOCCO, KICHUYA




SIMBA leo Jumamosi asubuhi, inatarajiwa kusafiri kwenda Songea kuwafuata Majimaji ambapo itaondoka bila ya mastaa wao, Emmanuel Okwi raia wa Uganda, Shiza Kichuya na John Bocco.

Simba inatarajiwa kuvaana na Majimaji FC katika mechi ya kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara itakayopigwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea, keshokutwa Jumatatu ikiwa tayari imeshatwaa ubingwa wa ligi hiyo, hivyo mchezo huo hawajautilia nguvu sana.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, wachezaji wa kikosi cha kwanza waliotumika kuipa ubingwa timu hiyo, wote hawaendi na timu kwa ajili ya mapumziko akiwemo Okwi na Bocco.

Mtoa taarifa huyo alisema msafara huo unatarajiwa kuwa na wachezaji 17 pekee pamoja na benchi la ufundi.

“Katika msafara wetu wachezaji ambao wakongwe watakaosafiri ni Niyonzima (Haruna), Mzamiru (Yasin) na Ndemla (Said) pekee, wengine waliobaki watakuwa ni vijana wa U20.

“Akina Bocco, Okwi na Kichuya (Shiza), Kwasi (Asante) na wengine waliotumika katika kikosi cha kwanza, wote watabaki kwa ajili ya mapumziko,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa mjumbe wa kamati ya utendaji wa timu hiyo, Said Tulliy kuzungumzia hilo, alisema kuwa “Ni kweli timu inasafiri kesho (leo) Jumamosi asubuhi kuelekea Songea kwa ajili ya mechi na Majimaji, lakini kuhusu kikosi kitakachokwenda benchi la ufundi ndio linajua.”

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.