Okwi: Tutampa furaha Magufuli
MSHAMBULIAJI tegemeo wa Simba na kinara wa kupachika mabao msimu huu, Emmanuel Okwi, amesema kuwa watahakikisha wanashinda mechi dhidi ya Kagera Sugar na kukabidhiwa kikombe cha ubingwa kwa furaha na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.
Okwi, alisema kuwa licha ya kutwaa ubingwa wakiwa na mechi tatu mkononi, wao walijipanga kusaka ushindi katika mechi 30, hivyo hawatakuwa tayari kuona wanapoteza mchezo huo wa kesho.
Okwi alisema kuwa wamejiandaa kukutana na ushindani na changamoto katika mechi hiyo, lakini ndoto za kutimiza malengo waliyoyaweka ya kutofungwa katika msimu huu bado hawajamaliza.
"Tunajipanga kupambana, ili kuhakikisha tunashinda katika mechi zote mbili zilizobakia, hatutaki kuona tunakabidhiwa kombe bila furaha, bado hatujamaliza kazi, ligi haijamalizika hivyo kila mechi kwetu tunahitaji kupata ushindi," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda na Yanga ya jijini.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma, amesema kuwa wanafuraha kutwaa ubingwa kabla ya mechi ya mwisho, lakini mazoezi yao yanaendelea kwa kasi ile ile waliyoanza nayo wakati msimu huu unaanza
"Kila timu inaingia uwanjani kwa ajili ya kusaka ushindi, ila kila mmoja akiwa na malengo tofauti, sisi sasa hivi tunasaka rekodi ya kutofungwa ambayo ilishawahi kuwekwa na klabu hii miaka ya nyuma," alisema kocha huyo raia wa Burundi.
Simba itaikaribisha Kagera Sugar ambayo tayari imeshajinasua katika janga la kushuka daraja ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 2-0 kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika Bukoba.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.