Okwi ajivunia kurejea Simba
MSHAMBULIAJI wa kimataifa na tegemeo wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/18, Emmanuel Okwi, amesema hajutii uamuzi wake alioufanya wa kurejea katika klabu hiyo.
Okwi ndiye mshambuliaji anayeongoza kwa kupachika mabao msimu huu, akiwa na mabao 20 na katika orodha hiyo anafuatiwa na nahodha wa Simba, John Bocco.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Okwi, alisema mbali na kupata ubingwa, anafurahia maisha ya ushirikiano na wachezaji wenzake ambayo ameyapata msimu huu.
Okwi alisema bado timu yake inajipanga kuhakikisha inaweka rekodi ya kufanya vizuri msimu huu, ikiwa imebakia na mechi moja mkononi ambayo ni dhidi ya Majimaji itakayopigwa Songea mkoani Ruvuma Machi 28, mwaka huu.
"Najivunia kuwa sehemu ya timu hii yenye njaa ya mafanikio, tuongeze umakini ili tutimize malengo yetu, lengo letu kubwa ni kuwapa furaha mashabiki pendwa wa Simba," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda.
Okwi, straika tegemeo pia wa timu ya Taifa ya Uganda (Cranes), ambaye amezaliwa Desemba 25, 1992, aliwahi pia kuichezea Yanga na baadaye kwenda Sweden.
Baada ya kusajiliwa na Simba mwaka jana, Okwi, Bocco, Shomary Kapombe na Erasto Nyoni wapinzani wao, Yanga waliwatania wamesajili wazee, lakini ndio wamesaidia kwa kiasi kikubwa kuipa timu yao ubingwa wakiwa na mechi tatu mkononi.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.