Mkude Aweka Rekodi Kubwa Simba sc.
Kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude amefanikiwa kuandika rekodi ya pekee klabuni hapo baada ya juzi Alhamisi timu hiyo kutangaza kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Simba ilitangaza kuwa mabingwa wapya ligi kuu msimu huu baada ya Yanga iliyokuwa ikichuana na timu hiyo kuwania ubingwa huo kufungwa na Prisons mabao 2-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliyofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Rekodi hiyo ya pekee ambayo Mkude ameiandika klabuni hapo ni ile ya kuwa mchezaji pekee aliyefanikiwa kunyakua ubingwa wa pili wa ligi kuu akiwa na timu hiyo bila ya kuhama ndani ya kikosi hicho.
Nyota wengine waliochukua ubingwa mara mbili na klabu hiyo lakini wao waliwahi kuhama kwa nyakati tofauti ni Mganda, Emmanuel Okwi, wazawa Mwinyi Kazimoto na Shomari Kapombe. Mara ya mwisho Simba ilikuwa imechukua ubingwa msimu wa 2011/12.
Mkude alisema kuwa: “Nimefurahi sana na ninamshukuru Mungu kwa hilo kwani nilipambana kwa muda mrefu kwa ajili ya mafanikio hayo lakini sasa ndoto zangu zimetimia.
“Nawashukuru sana viongozi wangu, wachezaji wenzangu pamoja na mashabiki wote wa Simba kwa ushirikiano mkubwa tuliokuwa nao msimu huu, nimuombe Mungu tu aendelee kutujalia hali hii ya ushirikiano iendelee katika mechi zetu zilizobakia lakini pia katika misimu mingine yote,” alisema Mkude.
CHANZO: CHAMPIONI
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.