Masau Bwire - Mzalendo: Hongereni Simba Sc-Mabingwa wa VPL-2017/18
Ni wachache sana washindanao, wapiganao, kupongezana baada ya mapambano, mshindwa akimpongeza mshindi kwa ushindi alioupata, mshindi naye akimpongeza mshindwa kwa namna alivyopambana kwa ushindani wa kweli japo alishindwa.
Mimi binafsi, kwa niaba ya Ruvu Shooting nichukue nafasi hii kuipongeza Simba sc, kwa kutwaa ubingwa wa VPL, msimu huu wa 2017/18, naamini, pamoja na hili na lile, mlistahili kuwa mabingwa, hongereni sana mabingwa.
Sisi Waswahili, tunasema, :nyota njema, uonekana asubuhi', ninyi msimu huu wa ligi mlionekana si tu asubuhi bali asubuhi sana, ni rudie kusema, hongereni mabingwa wa VPL, 2017/18, Simba sc, hongereni sana!
Nakumbuka, japo sitaki sana nikumbuke, asubuhi yenu msimu huu ilianza kuonekana uwanja wa uhuru, mapema kabisa, mchezo wa awali, wa ufunguzi wa ligi, sitaki kusema ilitokea nini, maana najua, wenye kumbukumbu, wanakumbuka, kuwakumbusha ni kuwapotezea muda, lakini kwa kweli, ubingwa ulianzia hapo!
Matokeo ya mchezo ule, leo niseme hadharani, yalinitesa, yaliitesa familia yangu, yalimtesa sana Mama yangu mzazi, Nyakwesi Mabamba Bwire (Marehemu), ambaye kwa wakati huo alikuwa kitandani, mgonjwa sana!
"Mama, kesho tunacheza na Simba ya Kariakoo, naitazama haina makali yale ya Simba wa porini, nakuahidi Mama, tutapata ushindi, tuko vizuri, Simba huyu sisi tutamfukuza tu kwa bakora, hatutatumia silaha kubwa, bakora tu itatosha kumuangamiza, halafu Mama, Kariakoo siku hizi hakuna mapori, Simba wote wakali, wararuao hawapo, ipo tu midoli, mifano ya Simba inauzwa maduka ya Wahindi kwa ajili ya watoto kuchezea, tutakupa faraja Mama, dakika 90 zitatosha kuikusanya Simba-midoli yote ya Kariakoo na kuwagawia bure watoto wa maeneo ya Kariakoo", maneno niliyomwambia Mama yangu nilipozungumza naye kwa simu, siku moja kabla ya mchezo huo!
Mama yangu kwa shida sana, maana alikuwa anaumwa sana, yuko tu kitandani alisema maneno haya, taratiiiibu na kwa upole, "haya, utanipa natokeo baada ya mchezo, mkishinda nitashukuru na kufurahi sana, maana nakupenda mwanangu, naipenda timu yako".
Unadhani kwa matokeo yale na hali ya ugonjwa aliokuwa nao Mama yangu, ilikuwa rahisi kumpa taarifa baada ya dakika 90 na kilichojiri 'Shamba la Bibi', ndo maana nasema, matokeo yale yalinitesa, pia yaliitesa familia yangu, sitayasahau, nimeyaweka kumbukunbu ya kudumu katika historia ya maisha yangu!
Simba, nyie nanilii ya Karikoo, mlinitesa sana, sikuwa hata na dalili za presha, hata kidogo lakini, tangu mchezo huo ambao niliuangalia kwa dakika 30 za nwanzo kisha, nikajifungia katika chumba cha wachezaji kubadilishia nguo hadi dakika 90 zilipomalizika, moyo wangu umekuwa ukiuma na kushtukashtuka!
Matokeo ya mchezo ule yalinipa taabu mno, wengine walijaribu kunipachika majina kuchagiza matokeo hayo, niliitwa kwa jina la kinywaji cha soda, '7 up' kiasi kwamba, walipokuwa wakienda dukani kununua kinywaji hicho, badala ya kukiomba kinywaji chenyewe kwa jina lake, waliomba wapatiwe 'Masau Bwire' bariiiiiiiidiiiii, wakimaanisha soda ya 7 up!
Simba nyie, hongereni kwa ubingwa, lakini, mmenitesa sana, kwa msemo wa vijana, kwa maumivu mlioniumiza, "Mungu anawaona"!
Rai yangu kwenu, jitahidini mmalize ligi bila kupoteza mchezo ili muandike historia nzuri kwa ligi ya msimu huu, uongozi uliopo uvunje rekodi ya mzee Dalali aliyoiweka enzi za uobgozi wake!
Mkipoteza mchezo katika michezo hii iliyosalia, itapunguza radha ya ubingwa kiasi fulani, maana tutaamini kwamba, mbali nanyi walikuwepo wengine bora zaidi kuwa mabingwa ndio maana wakakufungeni, lakini msipopoteza mchezo, hamuoni itakuwa raha kuusherehekea ubingwa kwa namna ya kipekee kwamba, mlikuwa bora zaidi ya timu zote, ndo maana hakuna timu iliyopata pointi tatu kutoka kwenu! Hongereni sana Mabingwa, mlistahili kuwa mabingwa!
Lakini pia, niwatake mjiandae vema, mjipange sawa sawa kwa ajili ya mashindano ya Kimataifa, ushiriki wenu ukaoneshe kweli kwamba, ubingwa wenu msimu huu ulitokana na uwezo na sio vinginevyo, mkafanye vizuri kimataifa, mtuaminishe Watanzania kwamba, ubingwa mliotwaa mlistahili, haukutokana na figisu na ile habari ya "kitu kidogo'
"Klabu bingwa katika ligi ya Tanzania na zile zinazoshuka daraja, haitokani na uwezo wa kimpira, ni figisu tu, ndo maana katika mashindano ya Kimataifa, timu hazifiki mbali kwakuwa ubingwa hawakuupata kwa uwezo bali figisu, wanapokwenda kimataifa, wanakutana na wenye uwezo, ni kipigo tu!" alisema Mtanzania mmoja.
Ebu katika ushiriki wenu wa Kimataifa, unesheni uwezo, fanyeni vizuri, mtuletee heshima ya soka la Kimataifa ndani ya nchi yetu, mfute kauli hizo za ubingwa wa figisu pasipo uwezo, zilizoganda katika baadhi ya vichwa vya Watanzania!
Nilitamani nimpe taarifa za ubingwa wenu Mama yangu, nimwambie kwamba, wale waliotunyima raha siku ile pale uhuru, ndio mabingwa, siyo sisi tu tuliowashindwa, hakuna hata mmoja aliyewaweza hivyo, tuendelee na maisha, tumepigwa wengi, kipigo cha wengi hakiumizi, lakini, Mama hayupo, ametangulia mbele za haki, alinipenda, aliipenda Ruvu Shooting, aliupenda Ruvu Shooting, amelala Mama yangu usingizi wa mauti, pumzika kwa amani Mama, nilikupenda sana, lakini, mapenzi ya Mungu hakuna mwenye uwezo wa kuyazuia, PUMZIKA kwa AMANI Mama.....
Mama aliipenda Ruvu Shooting, kwa hiari yangu, niseme bayana, itanichukua muda sana kuiacha Ruvu Shooting, kuendelea kudumu kuwepo Ruvu Shooting ni sehemu ya kumuenzi marehemu Mama yangu kwa aliipenda Ruvu Shooting.
Nimefuatwa na klabu kadhaa zenye uwezo wa kifedha, waliniahidi fedha nyingi ili nikatumike kwao lakini imekuwa ngumu mimi kubanduka Ruvu Shooting kutokana na mapenzi yangu ya dhati kwa timu hiyo, lakini zaidi sana mapenzi ya Mama kwa Ruvu Shooting, ngoja nimuenzi Mama yangu kwa vitendo, ndani ya Ruvu Shooting.
Mama alifariki Machi 5, na kuzikwa Machi 9, 2018, ushiriki wa Ruvu Shooting ulikuwa mkubwa sana katika msiba huu, pamoja na wadau wengine wa soka, wakiwemo Azam fc, Ruvu Shooting walinifariji sana!
Siku aliyozikwa Mama, Ruvu Shooting walicheza na Singida utd, Namfua, mbali na matokeo ya 1-1 nilifarijika sana kwa namna Ruvu Shooting walivyompa heshima Mama yangu mzazi, kwanza, wachezaji wote walifunga vitambaa vyeusi, kabla ya mchezo walisimama dakika moja kumkumbuka Mama yangu, lakini stahili waliyoitumia kushangilia goli la Isa Kandulu ilionesha msiba wa Mama, hakika Ruvu Shooting, hawanilipi fedha kubwa, lakini wananithamini, wananipenda, nitawapenda, sitawaacha kwasababu ya kufuata mamilioni ya fedha huko kwingine, heshima na utu kwangu mimi ni zaidi ya mamilioni ya fedha.
Young Africans (Wa Kimataifa), mmepoteza ubingwa, msiumie sana, msitafutane uchawi, jiandae, jipangeni mapema kwa msimu ujao kwani, 'kutesa kwa zamu'
Watawakejeri, watawatusi, watawasema watakavyo, furahini tu kwa yote, ni utani tu huo wa watani kwa wao wamesota zaidi ya msoto wenyewe japo kwa sasa kwasababu wamepata, watajisahaulisha lakini, wamesota, na wao (Simba), wanajua wamesota kweli kweli, ni wakati wao, ngoja watese. Msijisahaulishe kuwapongeza kwa ubingwa, wapongezeni tu, ndo mabingwa, hakuna namna, tuwapongeze.
Ruvu Shooting moja ya mechi zilizobaki ni dhidi ya mtani wa Mabingwa, tuwape taarifa mapema, 'tunapapasa' siku hizi, mjipange kwa hilo, May 25, 2018, tunakuja Taifa "kuwapapasa" tuna hamu sana na ninyi, raha sana, 'kumpapasa' mtu mzima.
Simba Sc, hongereni sana, mlistahili ubingwa, tukumbukane tu mwaliko wa sherehe!
Masau Bwire - Mzalendo
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.