YANGA INAKIMBIA, SANGA ANATEMBEA
Nampenda Makamu Mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga, Nampenda sana. Ni mtu mtaratibu na muungwana. Huyu ni miongoni mwa viongozi wachache tulionao katika soka letu waliokosa makeke mbele ya kamera za waandishi. Ni nadra sana kumuona akizungumza kwa kuropoka mpaka mishipa ya shingo kumsimama.
Katika muda wake mdogo anaoutumia kuzungumza na Wanahabari, huzungumza masuala ya msingi tu. Sijawahi kumsikia akiwatania Simba hata kwa bahati mbaya, japo ni kawaida Simba na Yanga kutaniana. Si ajabu hata baadhi ya mashabiki wa Yanga hawamjui. Sanga ameamua kuishi hivi.
-Licha ya ukimya wake kunivutia, lakini hivi sasa uchangamfu wake kama kiongozi wa juu wa klabu unahitajika. Yanga wanapitia njia ngumu. Timu ina lundo kubwa la wachezaji wenye majeraha. Timu imeshakosa taji la Ligi Kuu Bara. Timu inatajwa kuwa na ukata wa fedha, Sanga anakaaje kimya kana kwamba hali ya klabu nzuri na inavutia?
Kauli yake ni kama chafya kwa mpishi inavyoweza kuleta nafuu kwa mlaji chakula. Natamani atokeze na kusema lolote lile ambalo litawafariji Wanayanga wanaoishi kama kinda la ndege linalosubiri chakula cha mama yake ndani ya kiota bila kujua mama mwenyewe atarudi muda gani.
-Hali ya timu kila mmoja anaijua, sio siri tena. Lakini ukimya wake kama mtu wa juu wa klabu unaleta maswali mengi yaliyokosa majibu. Huu ndiyo ulipaswa kuwa muda wake wa kukaa chini na kuchora ramani ya vita ili Yanga iweze kusonga, sio kukaa kimya. Ukimya wake na upole alionao auweke kando kwa masilahi mapana ya Yanga.
Wakati mwingine unatakiwa kujivisha ngozi ya chui ili maisha yasonge. Sibezi au kucheka, lakini ni hatari Yanga kucheza mechi na benchi lake wakakaa wachezaji wawili. Ndanda Fc, Njombe Mji , Majimaji zenye hali mbaya hatujawahi kuziona zifikia hatua hii katika michezo yake.
Kama Sanga hajalitazama kwa macho matatu tukio lile la Mbeya kuna siku Yanga wataingia uwanjani na wachezaji saba. Ina maana Yanga ndiyo imefikia hivi? Serious, siamini nilichokiona.
Charles Boniface, Dismas Ten, Salum Mkemi, Hussein Nyika ni kama wamesusiwa timu ki'dizain'. Hawa ndiyo wanaotokeza kila mara kuilinda image ya klabu, lakini Makamu Mwenyekiti yuko kimya mno Tena mno Mno kabisa.
Kama kumbukumbu zangu ziko vizuri mara mwisho kumuona Sanga mbele ya kamera za waandishi akiwa Yanga ni siku aliyokuja kumtambulisha kocha George Lwandamina. Kumbukumbu zangu zinaniambia hivi. Kama kuna mtu anajua zaidi ya hapa anikumbushe.
Inawezekana kukawa na vikao vya siri baina ya viongozi na Makamu Mwenyekiti, lakini bado kauli ya hadharani ya Sanga ni nzito kuisikia ikipenya kwenye masikio ya mashabiki na wanachama, kuliko kwa viongozi walioko chini yake. Anatakiwa kutoka hadharani na kuzungunza. Hakuna namna.
Najua Sanga ana majukumu mengine ya Bodi ya Ligi ( TBLP) akiwa kama Mwenyekiti, lakini hii haimfanyi akose muda wa kuitisha Mkutano na Waandishi ili kutoa kauli juu ya mwenendo mzima wa klabu na nini klabu inataka kufanya kuondoa hali iliyoko.
Huruma iliyoje kwa Ten, Mkwasa, ni wao kutwishwa zigo la kujibu kila swali kuhusu timu, wakati kuna maswali mengine yanatakiwa kujibiwa na Sanga. Anyway muda huu ambao Simba wamekuwa mabingwa tayari, huku wakiwa na michezo mitatu mkononi, Sanga anapaswa kujua unapocheza ngoma tazama na jua.
Na Abdul Mkeyenge
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.