CAF Yafanya Mabadiliko Ya Ratiba Ya Klabu Bingwa Na Kombe la Shirikisho.

Michuano ya ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho ya msimu ujao itaanza mwaka huu mwezi Disemba na kumalizika mwezi Mei 2019 kulingana na mabadiliko yaliyofanywa na Shirikisho la soka Barani Afrika, CAF.

CAF imebadili kalenda ya michuano hiyo ambayo imekuwa ikianza mwezi Februari hatua ya awali na kumalizika mwishoni mwa mwezi Novemba.

Aidha baada ya kipindi cha mpito, kuanzia msimu wa 2019/20, michuano hiyo itakuwa ikianza mwezi Septemba na kumalizika mwezi Mei kama ilivyo michuano kama hiyo Barani Ulaya. 

Klabu ya Simba ndiyo itakayoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa itakayoanza Disemba baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa VPL wakati mwakilishi wa kombe la Shirikisho atafahamika Juni 02 baada ya mchezo wa fainali kati ya Singida United dhidi ya Mtibwa Sugar.

Hata hivyo Singida United huenda ikachukua nafasi hiyo kwa kuwa Mwaka 2003 Mtibwa Sugar ilifungiwa na CAF kutoshiriki michuano yoyote inayosimamiwa na shirikisho hilo kwa miaka mitatu kutokana na kushindwa kwenda kucheza dhidi ya Santos FC ya Afrika Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Tangu mwaka 2003 Mtibwa Sugar haikuwahi kufuzu kwa michuano hiyo huku wengi wakitafsiri kuwa adhabu hiyo inahusisha miaka ambayo klabu hiyo imefuzu.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.