Wanne Njombe Mji Waondolewa Kikosini Kwa Utovu Wa Nidhamu
Klabu ya soka ya Njombe Mji imewasimamisha kwa muda na kuwarudisha mkoani Njombe wachezaji wanne kwa kile kilichotajwa kuwa ni kutokana na utovu wa nidhamu.
Akiwataja wachezaji hao katibu mkuu wa Njombe Mji Obedy Mwakasungura amesema ni pamoja na Mlinda mlango namba moja David Kisu, Awadhi Salumu, Joshua John na Peter Mwangosi.
"Tumewaondoa kikosini na kuwarudisha kambini, tumeona kwamba hatuwezi kuendelea nao na safari kwenda Mwanza kutokana utovu wa nidhamu waliouonesha, nafikiri baada ya kurejea Njombe tutakaa na kamati tendaji na kutoa uamuzi kuwahusu," Mwakasungura amesema.
Maamuzi hayo yanakuja siku moja tu toka Njombe Mji wapoteze kwa mabao 3-1 kutoka kwa Stand United kwenye mchezo wa ligi ambao umefanyika Jumapili kwenye uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Katika mchezo huo wachezaji wawili kati ya hao wachezaji wanne walitumika isipokuwa kwa Joshua John na Kipa David Kisu ambaye amekuwa tegemeo kwa michezo ya hivi karibuni.
Aidha maamuzi hayo yanatolewa wakati ambapo Njombe Mji wapo katika hali mbaya kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na alama 18 katika nafasi ya 15 huku wakiwa na michezo saba mkononi.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.