Okwi, Simba washindikana ,Wakalia kileleni, straika huyo akigeuka lulu baada...



SIMBA na mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi, wamezidi kung'ang'ania kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na orodha ya wafungaji bora, baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar lililofungwa na straika huyo raia wa Uganda.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Jamhuri mkoani hapa, bao hilo pekee lilifungwa na Okwi, katika dakika ya 25 akimalizia pasi ya John Bocco, hivyo kumfanya Mganda huyo sasa kufikisha mabao 17 msimu huu.

Kwa idadi hiyo, Okwi sasa anawaacha mchezaji mwenza wa Simba, Shiza Kichuya na Obrey Chirwa wa Yanga kwa mabao matano katika mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu Bara msimu huu.

Kadhalika, kwa upande wa Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, imefikisha pointi 52, sita mbele ya Yanga iliyopo nafasi ya pili, lakini ikiwa na mechi moja mkononi.

Baada ya mechi hiyo  kumalizika jana, mashabiki walipagawa kwa kuimba na kushangilia huku wakimtaja Okwi...Okwi...Okwi...

Hata hivyo, Simba ilipoteza nafasi nyingine ya kupata bao katika dakika ya 28 baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Bocco kutoka nje.

Dakika ya 35, Mtibwa Sugar walijibu shambulizi hilo kupitia kwa Ismail Mhese ambaye alipokea pasi kutoka kwa Hassan Dilunga, lakini shuti lake lilipaa juu.

Okwi naye alipoteza nafasi ya kufunga bao sekunde chache kabla ya kwenda mapumziko baada ya kung'ang'ania mpira badala ya kutoa pasi na badala yake shuti hafifu alilopiga kudakwa na kipa wa Mtibwa Sugar, Benedict Tinocco.

Hadi wanakwenda mapumziko katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Aboubakar Mturo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kilichoko Mtwara, na wakicheza katika mvua kwenye vipindi vyote viwili, Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.

Baada ya mechi hiyo ya jana, Simba inarejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa kuwakaribisha Mbeya City katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayopigwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa.

Mtibwa Sugar; Benedict Tinocco, Kibwana Shomary, Hassan Mganga, Dickson Daudi, Hassan Isihaka, Shabani Nditi, Salum Kihumbwa, Henry Joseph, Stamil Mbonde/Hussein Javu (dk. 63), Hassan Dilunga/Ayoub Semtawa (dk. 73) na Ismail Mhessa/Haroun Chanongo (dk. 65).

Simba; Aishi Manula, Nicholas Gyan/Haruna Niyonzima (dk. 76), Asante Kwasi, Paul Bukaba, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin/Salim Mbonde (dk. 67), Shomary Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya.


Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.