Simba wala kiporo na ndimu
Timu ya soka ya Simba Sports Club ya jijini Dar es Salaam imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Njombe Mji, katika mchezo wa kiporo wa ligi kuu soka Tanzania Bara ambao umefanyika kwenye uwanja wa Sabasaba Mjini Njombe.
Katika mtanange huo, Simba waliuanza mchezo kwa kasi na ndani ya dakika ya 10 za mwanzo tayari walikuwa wameshakosa nafasi mbili za wazi kwanza ni John Bocco ambaye shuti lake lilipaa juu, huku Emmanuel Okwi akishindwa kuonganisha majaro yaliyochongwa na Nicholas Gyan.
Bao la Bocco
Kwa kasi hiyo Simba walifanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika ya 17 kupitia kwa John Bocco ambaye alimpiga chenga mlinzi wa Njombe Mji na kugeuka kwa kasi na kupiga shuti kali nje ya 18 lililomshinda mlinda mlango David Kisu na kujaa wavuni.
Hadi timu zinakwenda mapumziko Simba walikuwa mbele kwa bao moja ilihali Njombe Mji ambao ndio wenyeji wa mchezo huo wakiwa nyuma licha ya kupoteza nafasi kadhaa za kusawazisha bao hilo.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Simba walifanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa Emmanuel Okwi na kumuingiza Laudit Mavugo baada ya takribani dakika tano kuonekana kushindwa kulikaribia lango la Njombe Mji.
Aidha beki Salim Mbonde ambaye alikuwa na majeruhi kwa muda mrefu aliingia katika dakika ya 60 kuchukua nafasi ya James Kotei baada ya kuumia wakati akiwania mpira na mchezaji wa Njombe Mji.
Bao la Pili
Licha ya mpira kutokuwa na mvuto sana toka kuanza kwa kipindi cha pili, Simba walifanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya 64, kupitia kwa yule yule John Raphael Bocco akiwa pekee yake alimchambua kipa David Kisu baada ya kupokea pasi kutoka kwa mlinzi Shomari Kapombe
Baada ya bao hilo Njombe Mji walifanya mabadiliko kwa kumuingiza Raphael Siame kuchukua nafasi ya Etienne Ngiladjoe, lengo la kocha Ally Bushiri likiwa ni kuwapunguza kasi Simba ambao walianza kuelewana wakitafuta bao la tatu.
Washambulliaji wa timu zote mbili waliendelea kukosa nafasi za wazi za kupachika, jambo ambalo liliwafanya makocha wote kufanya mabadiliko kwa Njombe Mji walimtoa Stephen Mwanjala na nafasi yake kuchukuliwa na Agaton Mapunda huku Simba wakimuingiza Haruna Niyonzima na kumtoa Shiza Ramadhan Kichuya.
Matokeo hayo yanawafanya Simba kufikisha alama 49 na kujikita kileleni kwa tofauti ya alama 3 na wapinzani wakubwa Dar Young Africans ambao wao wanaalama 46 katika nafasi ya pili, huku kila timu ikiwa imekwishacheza michezo 21 katika msimu wa huu wa ligi kuu Tanzania Bara.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.