Mshambuliaji Stars Aahidi Kuwaondoa Zambia
Mshambuliaji mkongwe wa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) Asha Rashid 'Mwalala' amewatoa hofu watanzania na kuwapa moyo kuwa watafanikiwa kuwaondoa Zambia (She-Polopolo) watakapokutana katika mchezo wa marudiano kufuzu kwenye fainali za Mataifa Afrika kwa upande wa wanawake (AWCON).
Mwalala amesema sare ya mabao 3-3 waliyoipata imechangiwa na wao kujiamini sana walipokuwa wakiongoza kwa mabao 3-2 kwa muda mzima wa kipindi cha pili na kusahau kushambulia lakini Mwalimu atakuwa ameona mapungufu yao na atayafanyia kazi kabla ya mchezo huo.
"Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa ambayo wao wameyatumia na kutoka nyuma na kusawazisha, tutakapokwenda kwao tutayarekebisha kwani tayari walimu wameyaona, tatizo tulikuwa tayari tumeshajiamini, tulitakiwa pale tuliposhinda tuongeze juhudi zaidi, ila nafasi ya kusonga mbele ipo lazima tufudhu hatua inayofuata," amesema.
Mwalala amefunga mabao mawili kati ya mabao matatu yaliyofungwa na Twiga Stars katika mchezo huo, ambapo bao lingine limefungwa na Stumai Abdallah katika dakika ya kwanza kabisa ya mchezo huo uliofanyika Jumatano katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Upande wa Zambia
Kwa upande wa mfungaji wa mabao mawili ya Zambia Babra Banda, amekisifu kikosi cha Twiga Stars lakini ametoa tahadhali kuelekea katika mchezo ujao wa marudiano, utakaofanyika mjini Lusaka.
"Tanzania walikuwa na timu nzuri, tulipokwenda kwenye mapumziko niliwaambia wenzangu kuwa tunatakiwa kushambulia, na tulitulia na kushambulia kwa kasi na kupata mabao, wanakuja kwenye uwanja wetu hatutawaruhusu kufunga bao, na mwalimu wetu tayari ameona wapi tunatakiwa kufanya," Banda amesema.
Ili Twiga Stars waweze kusonga mbele wanahitaji kuibuka na ushindi wa aina yoyote au sare ya mabao kuanzia manne na kuendelea pale watakaporudiana Jumapili ya April 8, 2018 katika uwanja wa Nkoloma uliopo katika mji wa Lusaka nchini Zambia.
Michuano ya mwaka huu ya Mataifa Afrika kwa upande wa wanawake itafanyika nchini Ghana kuanzia Novemba 17 hadi Disemba Mosi mwaka huu.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.