Mshambuliaji Mbao Fc Afurahia Kuitwa Timu Ya Taifa



Mshambuliaji wa timu ya soka ya Mbao ya Jijini Mwanza Habibu Haji Kyombo amesema hakuna siku ambayo amewahi kufurahi katika maisha yake ya soka kama siku alipopewa taarifa ya kuwa amejumuishwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes).

Habibu ambaye nyota yake imeanza kung'aa msimu huu amesema anajivunia kuona ameitwa kwa ajili ya kuipigania nchini yake kitu ambacho alikuwa anakiota kwa muda mrefu sasa.

"Unajua siku ambayo nimepewa taarifa hii nilifurahi sana, kila siku nilikuwa Naomba niitwe kwenye timu ya Taifa ili niwakilishe nchi yangu, hatimaye ndoto yangu imekuwa kweli, ninafuraha sana kiasi ambacho siwezi kuelezea, nimejiunga na wenzangu kambini na maisha ya kambi yanaendelea vizuri, nashukuru kwa kweli," Kyombo amesema.

Kyombo amesema sasa jukumu ambalo lipo mbele yake ni kumsikiliza kocha na kuhakikisha anaisaidia timu kuweza kufanya vizuri kwa kuifunga DR Congo katika mchezo wa marudiano na kusonga mbele katika kuwania tiketi ya kushiriki michuano ya Afrika kwa vijana itakayofanyika mwakani nchini Niger.

Kyombo hakuwepo kwenye mchezo wa ligi kati ya timu yake na Njombe Mji ambapo, Mbao FC waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao yakifungwa na David Mwasa na Rajesh Kotecha.

Kwanini kaitwa sasa?

Aidha mwalimu Ammy Conrad Ninje amezungumza na mtandao huu na kuuelezea sababu ya kumjumuisha Kyombo katika kikosi chake akiwa hakuitwa mwanzoni katika mchujo wa awali wa wachezaji 46.

"Unajua unapokuwa mwalimu lazima utafute maeneo mengi ya kusaidia kikosi chako, sasa sio kwamba wachezaji wote wa Tanzania waliitwa kwenye mchujo, kuna wengine walikuwa nje ya nchi, sasa Mimi kama mwalimu lazima niviangalie hivyo vipaji ambavyo vipo hata nje ya Tanzania, kusudi nipate timu imara na Ndio maana nimemuita Habibu na huyo mwingine," Ninje amesema.

Mbali na Kiyombo pia mchezaji mwingine ambaye anacheza soka nchini Senegal ameitwa katika kikosi hicho lakini kocha Ammy Ninje amesema atamuweka wazi mchezaji mara tu atakapowasili kwenye kambi.

Ngorongoro Heroes wapo kambini kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya DR Congo utakaofanyika April 22 ambapo kutokana na Suluhu waliyoipata nyumbani watahitaji ushindi au sare kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua inayofuata na kucheza na Mali.

Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.