Kumbe Uzembe wa Yanga Ndio Uliochangia Mtibwa Sugar kupata adhabu ya kutoshiriki michuano ya CAF
MTIBWA Sugar imetinga fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) maarufu kama Azam Sports Federation Cup ambalo mshindi wake hupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Lakini bahati mbaya kwao ni kwamba hawataweza kushiriki mashindano hayo hata kama watashinda ubingwa ubingwa huo ambao huambatana na zawadi ya Sh50 milioni.
Hii inatokana na adhabu waliyoipata mwaka 2004 kwa kushindwa kwenda kwenye mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya mashindano hayo hayo, dhidi ya Santos ya Afrika Kusini.
Kimsingi, adhabu hii ya Mtibwa Sugar ni zao la historia ya mpira wetu na inaonyesha ni wapi tumetoka ili turekebishe tulipo na tuboreshe tuendako.
Mzee wa upupu ninakuletea makosa matatu makubwa ya kihistoria yaliyosababisha Mtibwa Sugar kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika na hatimaye kufungiwa. Kwa kifupi kuna mbeleko fulani hivi ilitumika, twende pamoja.
KOSA LA KWANZA - UPENDELEO KWA YANGA SC
Wakati huo Tanzania ilikuwa na Ligi ya Muungano iliyokuwa ikitambuliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) na Shirikisho la Vyama vya Soka vya Kimataifa (Fifa) kama ligi rasmi na ndiyo iliyokuwa ikitoa bingwa wa taifa na wawakilishi kwenye mashindano ya Afrika. Ligi ya Bara na Ligi ya Zanzibar hazikuwa zikitambuliwa, hivyo bingwa wake aliishia kushiriki Kombe la Kagame tu.
Ligi ya Muungano ilianza mwaka 1982 na ilikuwa ikihusisha timu bora za juu kutoka Ligi ya Bara na Ligi ya Zanzibar. Mwanzoni zilikuwa timu mbili mbili na baadaye zikaongezwa na kuwa timu tatu kutoka kila upande wa Muungano.
Mwaka 2003, Yanga ilimaliza Ligi ya Bara kwenye nafasi ya nne hivyo haikufuzu kwa Ligi ya Muungano. Waliofuzu walikuwa mabingwa Simba, Tanzania Prisons walioshika nafasi ya pili na nafsi ya tatu ilichukuliwa na Mtibwa Sugar.
Lakini mamlaka za soka, FAT na ZFA, zikahofia Ligi ya Muungano kupooza endapo Yanga itakosekana, hivyo wakaipa nafasi ya upendeleo. Wakabadili kanuni za mashindano juu kwa juu na kuongeza timu shiriki kutoka tatu kila upande mpaka nne.
Yanga, namba nne wa Bara na Maendeleo, namba nne wa Zanzibar, zikafuzu kwa mujibu wa kanuni mpya.
Endapo Yanga asingepewa nafasi ya upendeleo kushiriki Lligi ya Muungano, idadi ya timu isingeongezeka na ligi isingepangwa kuchezwa kwa mtoano na Mahakama isingeisimamisha
KOSA LA PILI – FAT NA ZFA
Itakumbukwa mwaka huo, FAT ilikumbwa na migogoro mingi ukiwemo ule uliosababisha mwenyekiti wake, Muhidin Ndolanga na Katibu Mkuu, Michael Wambura kuondolewa madarakani na nafasi zao kuchukuliwa na mwenyekiti wa chama cha soka Mkoa wa Mtwara, Yahaya Mhata na Katibu Mkuu wa Chama cha Makocha TAFCA, Mwina Kaduguda.
Migogoro hii iliichelewesha Ligi ya Bara ambayo awali ilitakiwa imalizike mwishoni mwa Septemba au mwanzoni mwa Oktoba lakini ikamalizika mwishoni mwa Novemba (Nov 26).
Kuchelewa kumalizika kwa Ligi ya Bara kukachelewesha kuanza kwa Ligi ya Muungano. Lakini pia kuongezeka kwa timu shiriki kukaongeza muda wa mashindano kwa sababu idadi ya mechi nayo iliongezeka. CAF ilipanga Desemba 24, itakuwa siku ya mwisho ya kupokea majina ya wawakilishi wa kila nchi hivyo endapo Ligi ya Muungano ingechezwa kwa mtindo wa kawaida wa nyumbani na ugenini, isingemalizika kabla ya tarehe hiyo, hivyo Tanzania ingeshindwa kupeleka majina ya wawakilishi wao.
FAT na ZFA wakaamua ligi ya Muungano ichezwe kwa mtindo wa mtoano wakianzia na robo fainali Desemba 10, nusu fainali Desemba 12 na fainali Desemba 14.
Yanga ambao waliingia kwa ‘viti maalumu’ walipangwa kucheza na Jamhuri ya Pemba lakini wakagoma wakisema hawajawahi kuona ligi ya mtoano duniani. Ilisemekana wakati ule walishawishiwa na mwenyekiti wa FAT aliyeondolewa madarakani, Ndolanga, ili kuwaharibia viongozi wapya. (Inasemekana lakini). Hili lilitiwa nguvu na kitendo cha Yanga kutoa kauli hii wakati tayari ikiwa imeshafika Unguja. Yaani ilishaondoka Dar es Salaam kuelekea Pemba lakini ilipofika Unguja, ikagoma na kuja na hoja ya ‘duniani hakuna ligi ya mtoano’.
FAT na ZFA zikaipatia Jamhuri ushindi wa mezani lakini Yanga haikuishia hapo, ikaenda kufungua kesi kwenye Mahakama ya Ilala kwa Mheshimiwa Hakimu Agatha Kaguta.
Katika kesi hiyo ambayo ilifunguliwa na katibu mkuu wake, Jamal Malinzi, Yanga iliwalalamikia viongozi wa FAT kwa kutowasilikiza madai yao hivyo wakaitaka Mahakama iwahukumu vifungo jela viongozi hao.
Mahakama ikasimamisha Ligi ya Muungano na kupanga kuanza kuisikiliza kesi hiyo Februari 2004.
FAT na ZFA zikaona haziwezi kusubiri mpaka kesi isikilizwe, hivyo zikaamua kuwachagua mabingwa wa pande zote mbili kuiwakilisha nchi. Simba kama mabingwa wa Bara, ikachaguliwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, na Jamhuri ya Pemba, kama Mabingwa wa Zanzibar ikachaguliwa kushiriki Kombe la Shirikisho.
Endapo FAT isingekuwa na migogoro, Ligi ya Bara isingechelewa kuisha na hivyo Ligi ya Muungano isingechelewa kuanza.
KOSA LA TATU – UPENDELEO KWA MTIBWA SUGAR
Jamhuri na timu zote za Zanzibar, zikasema hazina uwezo wa kifedha, hivyo wakaomba wasipewe hiyo nafasi. Ndipo ZFA wakaichagua Mtibwa Sugar kutoka Bara ichukue nafasi hiyo lakini kwa masharti kwamba ichezee mechi zake Zanzibar.
Hapo ndipo Mtibwa Sugar ilipoitwa mtoto wa kambo wa Zanzibar. Mtibwa Sugar ikakubali lakini ilipoanza kushiriki mashindano hayo, ikagoma kuchezea Zanzibar badala yake ikachezea Dar es Salaam.
Katika mechi ya raundi ya awali, Mtibwa Sugar iliitoa Mumias Sugar ya Kenya kwa mabao 4-1, wakianza na ushindi wa 2-0 ugenini na 2-1 nyumbani. Ushindi huo ukaivusha hadi raundi ya kwanza ilipokutana na Santos ya Afrika Kusini. Ikafungwa 3-0 nyumbani na ilipotakiwa kwenda kwenye mechi ya marudiano jijini Cape Town, ikasema haina fedha.
Ndipo ilipokutana na rungu hili ambalo adhabu yake ilitakiwa kuhesabiwa kuanzia pale itakapofuzu kwa mashindano ya Afrika. Kuanzia mwaka huo mpaka sasa, Mtibwa Sugar haikuwahi kufuzu kwa mashindano yoyote ya kimataifa. Labda Kombe la Mapinduzi!
Endapo ZFA isingeipa Mtibwa Sugar nafasi ya upendeleo, badala yake ingeipa TZ Prisons ambayo ilimaliza juu ya Mtibwa Sugar kwenye Ligi ya Bara, huenda adhabu hiyo leo hii isingekuwepo.
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.