Batshuayi kukosa michezo iliyosalia Ujerumani
Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji anaeitumikia klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa mkopo Michy Batshuayi, atakosa sehemu ya msimu iliyosalia, kufuatia majeraha ya kifundo cha mguu yanayomkabili.
Mshambuliaji huyo ambaye aliuzwa kwa mkopo mwezi Januari kutoka Chelsea, alipatwa na majeraha hayo wakati wa mchezo wa ligi ya Ujerumani mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Schalke 04, walioibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.
Mshambuliaji huyo alilazimika kutolewa uwanjani na machela, kufuatia maumivu makali aliyoyahisi, jambo ambalo lilizua hofu kwa mashabiki wake.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa na Borussia Dortmund imeeleza kuwa, Batshuayi ana nafasi kubwa ya kuziwahi fainali za kombe la dunia, zitakazoanza Urusi Juni 14.
“Michy Batshuayi anaugulia maumivu ya kifundo cha mguu, lakini tuna matarajio makubwa ya kumuona tena uwanjani, na huenda akawa sehemu ya timu yake ya taifa itakayoshiriki fainali za kombe la dunia,” imeeleza taarifa ya Dortmund.
Batshuayi amekua na kiwango kizuri tangu alipohamia Dortmund, na mpaka sasa ameshafanikiwa kufunga mabao tisa katika michezo kumi na nne aliyocheza katika ligi ya Ujerumani
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.