Mayanja Awafunulia Simba Mbinu Za Kuimaliza Al-Masry.


STRAIKA wa zamani wa Al Masry ya Misri, Jackson Mayanja, ameipatia Simba mbinu zitakazoiwezesha kuibuka na ushindi katika mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaozikutanisha timu hizo.

Simba itacheza na Al Masry Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo huo wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

Mayanja alipata kutamba na Al Masry mwaka 1995 na kufanikiwa kuifungia mabao nane katika Ligi Kuu ya Misri na kuifanya timu hiyo imalize ligi hiyo katika nafasi ya nne.



Mayanja raia wa Uganda ambaye ni kocha msaidizi wa zamani wa Simba, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, wachezaji wa Simba wakicheza kwa kujituma na kwa nidhamu ya hali ya juu basi wataibuka na ushindi.

Alisema baada ya kupata taarifa kuwa Simba itacheza Al Masry aliifuatilia mwenendo wake katika ligi ya Misri na kubaini kuwa ni timu nzuri na inafanya vizuri kwenye ligi hiyo ila haina beki kwani mpaka sasa imefungwa mabao 24 katika mechi 24 ilizocheza.



“Kwa hiyo wachezaji wa Simba wanatakiwa kuingia katika mechi hiyo na kujituma vilivyo pia wakicheza kwa nidhamu ya hali ya juu hakika wataibuka na ushindi.



“Lakini kama watashindwa kufanya hivyo mechi itakuwa ngumu sana kwani wachezaji wa Kiarabu ni wajanja sana katika kucheza mechi za ugenini, kwa hiyo Simba wasiwaruhusu kabisa kumiliki mpira.

“Pia wacheze soka la kasi na kushambulia muda wote lakini kwa umakini na nidhamu ya hali ya juu,” alisema Mayanja.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.