Kipa Azam (Razak Abalora) Afungiwa Kwa Muda


Bodi ya ligi ya shirikisho la soka Tanzania Bara (TPBL) imemsimamisha kipa wa Azam, Razak Abalora kuichezea timu hiyo kwa kosa la kumtolea lugha isiyofaa mwamuzi Jonesia Rukyaa baada ya mechi dhidi ya Simba uliochezwa February 07 suala lake limepelekwa kamati ya nidhamu na maadili kujadiliwa. Abalora inadaiwa Baada ya Mpira kumalizika alimfuata Mwamuzi Rukya kumlalamikia kwa madai ya kuwanyia Penati.


Kwa mujibu wa barua kutoka bodi hiyo iliyotumwa usiku Ijumaa kwa klabu hiyo, inaeleza kuwa Abalora anasimamishwa akidaiwa kumtolea lugha chafu mwamuzi Jonesia Rukyaa, mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Simba uliofanyika Februari 7 mwaka huu.

“Katika mechi namba 135 dhidi ya Simba iliyochezwa Februari 7, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mchezaji wako Razak Abalora alimtolea lugha chafu mwamuzi (Jonesia Rukyaa) baada ya filimbi ya mwisho,” ilieleza sehemu ya nukuu ya barua hiyo.

Aidha barua hiyo iliyoandikwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Boniface Wambura, iliendelea kueleza kuwa: “Kwa vile suala lake ni la kinidhamu, na kwa kutumia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imemsimamisha kucheza mechi za Ligi Kuu hadi suala lake litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).”

Barua hiyo ilimalizia kuwa, Abalora aliyesajiliwa akitokea WAFA FC ya Ghana atafahamishwa siku ya kikao cha kamati hiyo kusikiliza shauri lake ambapo pia ataruhusiwa kuwasilisha utetezi wake.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.