Habari Njema Kwa Mashabiki Wa Simba Kuhusu Hali Ya Niyonzima..



HII inaweza kuwa ni habari njema kwa mashabiki wa Simba baada ya nyota wao, Haruna Niyonzima aliyekuwa nje kwa muda mrefu akisumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu wa kulia, sasa karejea tena uwanjani.

Akizungumza jana, Niyonzima amethibitisha yupo fiti na ataanza mazoezi na wenzake mara watakaporejea kutoka Misri watakakokocheza keshokutwa Jumamosi mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry.

“Sasa niko fiti, naweza kurudi uwanjani, nadhani wenzangu watakaporejea kutoka Misri tu nitajiunga nao mazoezini,” alisema Niyonzima jana kwa furaha.


Kiungo huyo fundi ambaye alikubalika kwa mashabiki wa Simba alipojiunga na timu hiyo akitokea Yanga mwanzoni mwa msimu huu, alisema anarejea upya uwanjani na anaamini mambo yatakuwa mazuri tena kwake.


“Matatizo ni sehemu ya maisha, lakini nashukuru Mwenyezi Mungu amenisimamia na sasa nimepona na bila shaka nitarudi uwanjani mapema wenzangu watakaporejea nchini,” alisema.


“Naendelea na mazoezi binafsi, niko ‘bomba sana’ akimaanisha yuko fiti na bahati iliyoje sikufanyiwa upasuaji kama ilivyotarajiwa nilipokwenda India.


“Kule nilipewa matibabu mbadala na ninaendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu tiba imenisaidia na ninaendelea vizuri,” alisema kiungo huyo Mnyarwanda.


Akizungumzia matibabu yake India, Niyonzima alisema yalienda vizuri na alianza kupatiwa tiba mbadala iliyofanyika kwa siku 10 kisha madaktari wakabaini hana haja ya kufanyiwa tena upasuaji.


“Hilo lilikuwa jambo la kumshukuru Mungu pia, maana upasuaji nao ni kitu kingine, bahati nzuri tiba niliyopewa nje ya upasuaji imenisaidia na sasa niko tayari kurudi uwanjani,” alisema.


Kiungo huyo amekuwa na msimu mbaya tangu amejiunga na Simba akiwa hajafunga wala kusaidia bao lolote katika mechi chache alizocheza kabla ya kuumia.


Join us on WHATSAPP 
Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.