ISHU YA WAMBURA INAONYESHA NI JINSI GANI TFF ILIVYO
SOKA la Tanzania lilipata nafuu miaka kumi iliyopita pale lilipoanzishwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoka Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa nafuu yote ya soka letu imeanza kupotea tena.
Enzi za FAT, kiongozi angeweza kufanya taasisi hiyo kama yake akiamua kila kitu bila kumshirikisha yoyote na kutumia mwamvuli wa mambo ya soka kutopelekwa mahakamani. Tuliishi hivyo kwa miaka mingi.
Angalau afadhali ikaonekana baada ya Leodegar Tenga kuingia madarakani na kubadili mfumo mzima wa uongozi huku kamati zikifanya kazi zake kwa uhuru na haki bila kuegemea upande mmoja.
Mwaka wa mwisho wa uongozi wa Tenga, kamati zikaanza kujisahau na kutumia vibaya uhuru ziliopewa na TFF, mgombea wa urais wakati huo, Jamal Malinzi akawekewa mizengwe kibao hadi ilipoamuliwa mchakato uanze upya.
Malinzi akashinda na kuwa rais mpya wa TFF, lakini alipoingia madarakani mambo mengi yakaibuka tena ikiwemo ajira kutolewa bila kutangazwa ili wengi waombe. Hali ikarudi kama ya FAT na kiongozi akiamua jambo hakuna wa kupinga, tukavuka hivyohivyo.
Sasa limeibuka jambo lingine jipya ambalo ni msiguano wa viongozi wa juu wa TFF, Makamu wa Rais, Michael Wambura na TFF yenyewe. Madai mengi yametolewa kuhusu Wambura na tayari amefungiwa kujihusisha na soka maisha yake yote.
TFF inamtuhumu Wambura kupokea fedha za malipo ya TFF ambayo si halali, kughushi barua ya kuelekeza malipo kwa Kampuni ya Jeck System Limited na kuishushia hadhi TFF.
Wambura naye baada ya kutwishwa tuhuma hizo, akasema mambo mengi ikiwemo matumizi ya Sh Bilioni 3 bila maelezo ya kina na ajira za kirafiki ndani ya TFF. Kwa mkanganyiko huo Spoti Xtra tunaona hapa kuna tatizo.
Rais wa TFF, Wallace Karia lazima ajue anaongoza TFF yenye udhaifu mkubwa wa kiuongozi kutokana na namna suala hili la Wambura lilivyoenda na mambo yaliyoibuka. Wanaongoza soka la Tanzania huku wakiwa hawapendani na kauli rahis ni kwamba pale TFF wanaishi kinafiki.
Tunaona wazi kwamba Wambura ana udhaifu wake na TFF nayo ina uozo wao,tunaamini TFF ni taasisi kubwa na yenye nguvu lakini imeonyesha ina viongozi dhaifu wanaoweza kujibizana na Wambura mitandaoni bila kutumia utaratibu wa kisayansi wa kiofisi.
Kulikuwa na tatizo gani kwa TFF kumhoji Wambura halafu kumtia hatiani bila ya kumtangaza kwanza kwa umma halafu ndiyo ajadiliwe. Wapo watu wamejimilikisha soka la Tanzania na kuliona ni mali yao.
Kilio chetu siku zote ni kuhusu uzalendo lakini bado katika soka
wanachofanya viongozi wetu ni sawa na kile kilichokuwa kinafanywa miaka 11 iliyopita enzi za FAT.
Mambo mengi yameanza kwenda ndivyo sivyo jambo ambalo linazua wasiwasi.
Kwa sakata hili la Wambura inaonyesha wazi kuwa TFF sasa ina watu wa aina ile ya kubishana mitandaoni jambo ambalo hatukuliona kwa kiasi hicho enzi za Tenga na hii inamaanisha kwamba kuna watu ambao wako TFF kimakosa.
Ujuaji na ubinafsi ndiyo siku zote vinalemaza soka letu na wapo watu
wanaojifanya wenyewe ndiyo wenye maslahi na soka la Tanzania na kila panapoonekana kuna fedha lazima wawepo.
TFF itumie taratibu husika kumaliza tatizo lake na Wambura ambaye alikuwa bosi wa pili kutoka Karia katika taasisi hiyo nyeti ya soka nchini na hakuna haja ya kulumbana mitandaoni.
Hakukuwa na haja ya TFF kujibizana mitandaoni na mambo ya Wambura, badala yake ingetumia busara ya kulizungumza suala hili kwa kirefu na kwa undani halafu mambo mengine yangeenda kama walivyopanga.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.