Yanga Kushuka Dimbani Leo 'Nangwanda'

Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja kupigwa ambapo mabingwa watetezi, Yanga SC watakuwa wageni wa Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 

Huo ni mchezo wa kiporo wa mzunguko wa 19, ambao Yanga ilishindwa kuucheza kutokana na kukabiliwa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Saint Louis Suns United ya Shelisheli.

Na baada ya kuvuka Raundi ya Awali kwa ushindi wa jumla wa 2-1, ikishinda 1-0 nyumbani na sare ya 1-1 ugenini, Yanga inakuja kumalizia kiporo chake kabla ya kwenda kucheza mechi ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Lakini Yanga itateremka Uwanja wa Nangwanda jioni ya leo ikiwa kumbukumbu ya kutoshinda mechi nyumbani kwa Ndanda kati ya nne zilizotangulia, wakifungwa mbili na sare mbili.

Kwa ujumla, katika Ligi Kuu Yanga imekutana na Ndanda mara nane tangu timu hiyo ipande msimu wa 2014/2015 – huku mabingwa hao watetezi, wakishinda mechi tatu, kufungwa mbili na sare tatu. 

Yanga itajaribu kusaka ushindi wa kwanza leo Uwanja wa Nangwanda ikiwa inabakiliwa na wimbi la majeruhi klabuni.

Lakini hata Ndanda, hawapo katika ubora waliokuwa nao misimu miwili iliyopita, wakitoka kutolewa katika hatua ya 16 Bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) na kwenye Ligi Kuu kwenyewe wamevuna pointi 18 katika mechi 18 na wanalindwa na pointi tatu tu kuwa katika eneo la kushuka Daraja.

Yanga SC wanahitaji sana ushindi kwenye mchezo wa leo kupunguza idadi ya pointi wanazozidiwa na vinara, Simba SC katika mbio za ubingwa.

Wakiwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19, Simba SC wamesimama kileleni mwa Ligi Kuu, wakifuatiwa na mahasimu wao, Yanga pointi 37 za mechi 18.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.