Baada Ya Gendarmerie Hii Ndio Klabu Itakayokutana Na Simba Kombe La Shirikisho Afrika

Tokeo la picha la simba sc vs Al Masry
BAADA  ya ushindi wa jana timu ya Simba inatarajiwa kukutana  na timu ya Al Masry ya Misri, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba imefanikiwa kusogea mbele katika michuano hiyo baada ya kuwanyuka Gendarnerie Nationale Fc kwa juml ya magoli 5-0.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilishinda mabao 4-0 kabla ya jana kushinda bao 1-0.


Mchezaji wa kimataifa raia wa Uganda, Emmanuel Okwi alifunga bao hilo pekee dakika ya 53 katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali kwenye Uwanja wa State de Vile jijini Djibouti.


Kwa ushindi huo sasa Simba itacheza na Al Masry ya Misri iliyosonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-2, baada ya kufungwa 2-1 na Green Buffaloes ya Zambia.


Waarabu hao wakiwa na mshambuliaji hatari raia wa Burkina Faso, Aristides Bance katika mchezo wa kwanza nyumbani Cairo iliwafunga Wazambia mabao 4-0.


Mfumo wa Kocha Mfaransa Pierre Lechantre aliyeingia katika mchezo huo kwa mbinu ya kucheza kwa kujilinda akitumia mfumo wa 5-4-1, ulizaa matunda baada ya kudhibiti mashambulizi ya Gendarmarie.


Lechantre baada ya kuvuna mabao 4-0 nyumbani, aliamua kuanza mchezo wa jana akiwa na mabeki watano wa safu ya ulinzi ambao ni Juuko Murshid, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Yusufu Mlipili na Erasto Nyoni.


Beki kisiki Shomari Kapombe na kiungo mshambuliaji Said Ndemla walikuwa benchi, lakini Lechantre alibadili safu ya ushambuliaji kwa kumpanga Okwi peke yake bila pacha wake John Bocco.


Bocco alikuwa jukwaani katika mchezo huo kwa kuwa anakabiliwa na majeraha aliyopata katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mwadui Shinyanga.


Okwi alisaidiana na kiungo wa pembeni Shiza Kichuya kupeleka mashambulizi huku kiungo mkabaji Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na James Kotei wakitawala katika eneo la katikati.


Mkude, nahodha wa zamani wa timu hiyo mwenye uzoefu wa kutosha katika mashindano ya kimataifa, alicheza kwa ustadi na kuidhibiti Gendarmarie katika eneo la kiungo.


Kasi ya mchezo


Simba ilianza kwa kasi mchezo huo, lakini ilikuwa na tahadhari kubwa kwa kuwa ikitumia mfumo wa kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushitukiza.


Mfumo huo uliwalazimisha wanajeshi hao kufunguka na kutoa nafasi kwa Simba kuongeza kasi ya mchezo kabla ya kupata bao.


Okwi alifunga bao hilo kwa shuti baada ya kuchomoka na mpira kutoka winga ya kulia kabla ya kupiga mkwaju uliojaa wavuni.


Simba ilifanya mabadiliko dakika ya 62 kwa kumtoa Murshid na kuingia Moses Kitandu na dakika ya 77 alikwenda kwenye benchi Kichuya na kuingia kiungo mkongwe Mwinyi Kazimoto.


Pia Lachantre alifanya mabadiliko mengine katika kikosi hicho dakika ya 85 kwa kumtoa Mdhamiru na nafasi yake kujazwa na beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.