Mbaya wa Simba sasa atua Yanga


MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu ya kuanza kutabasamu kwa kile ambacho mabosi wao wamekuwa wakikifanya kwa sasa ili kuwapa furaha mitaani.


Ipo hivi. Mabosi hao wa Jangwani wanapambana na vita flani ya kimyakimya na sasa wamevunja benki ili kumshusha kocha aliyewatibulia Simba mbele ya Rais John Magufuli, lakini pia wakiamua kumrudisha kiungo Mcameroon aje kupiga kazi.


Yanga inataka kuboresha benchi lake na hali ya mambo haiwaridhishi mabosi wake hasa inapomkosa Kocha Mkuu, hivyo kuamua kufanya jambo la maana la kumleta Mecky Mexime kuja kusaidiana na Mkongo Mwinyi Zahera.


Yanga imekuwa ikitaabika tangu alipoondoka aliyekuwa kocha wao, George Lwandamina ikiwa imecheza jumla ya mechi 14 za ndani na nje ya nchi na kushinda moja tu dhidi ya Mbao ya Mwanza huku ikipoteza tisa na kutoa sare nne.


Muda wote Yanga ikitaabika ilikuwa chini ya makocha wasaidizi, Noel Mwandila na Shadrack Nsajigwa aliyetimka kikosini baada ya kubaini hana chake tena.


Kutokana na hali hiyo, mabosi hao wakanoa bongo zao fasta na kukubaliana kutafuta kocha fundi anayeweza kusimama hata kama Kocha Zahera akikosekana kikosini ndipo mipango yao ikatua kwa Mexime anayeinoa Kagera Sugar.


Yanga inamleta beki na nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars kuchukua nafasi ya Nsajigwa ambaye mkataba wake umemalizika.


Inaelezwa kuwa Mexime amekubalika hasa baada ya Zahera kuhitaji kocha msaidizi aliye mzawa na sio wa kigeni tofauti na ilivyokuwa ikifikiriwa mwanzoni alipoletwa Mkongomani Gay Bukasa ambaye hata hivyo alitimka baada ya Chama cha Soka cha DR Congo kumnyakua na kumpa mkataba mrefu ndani ya The Leopards.


Awali Mwanaspoti liliwahi kuvujisha mpango wa Yanga kubadili benchi lake na kumtambulisha Mexime na imekuwa hivyo.


Mabadiliko katika benchi la ufundi mpaka sasa yamemuacha salama Daktari wa timu tu ambapo daktari mkongwe Edward Bavu anadundadunda katika nafasi yake.


Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba mabosi wa Kamati ya Usajili na Mashindano wameshaanza mazungumzo na Kagera juu ya kumchukua Mexime.


Rekodi kubwa ambayo Yanga imewavutia kwa Mexime ni kutaka akili yake ya kutafuta wachezaji bora wazawa kama alivyofanya wakati akiwaibua winga Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Andrew Vincent Dante na wengine aliowapika akiwa Mtibwa Sugar akishirikiana na wakongwe wa Manungu.


Mbali ya hilo, pia rekodi nyingine iliyowavutia mabosi hao ni juu ya uwezo wa kocha huyo kuwasumbua watani wao Simba ambapo ni msimu uliopita tu aliwatia aibu Wekundu hao mbele ya Rais Magufuli alipowachapa bao 1-0.


Mechi hiyo ndio mchezo pekee ambao Simba iliupoteza msimu uliopita na kutibua rekodi yao ya kutaka kumaliza msimu bila kufungwa kama ilivyokuwa 2009-2010.




Kagera wapo freshi


Meneja wa Kagera Sugar, Mohammed Hussein, amekiri kusikia taarifa za kocha wao kutakiwa Yanga, japo kama meneja hajawahi kuwasiliana na kiongozi yeyote


wa Jangwani juu ya hilo, ila hawana kikwazo kwa vile Mexime ni mtu mzima.


“Yeye ndiye mwenye maamuzi ya kuvunja mkataba, hatumzuii kwa sababu ishu yake na ya wachezaji ipo tofauti, ila tumezisikia taarifa hizo na Kagera haiwezi kumzuia Mexime kwenda anakotaka, ingawa bado tuna mkataba naye,” alisema.


Naye Mexime alipotafutwa kwa njia ya simu, alikiri Yanga kumhitaji, ila akasema kwa ufupi; “Nasubiri majibu toka kwa mabosi wangu kuona inakuwaje.”




Kiungo Mcameroon arudishwa


Kwa wanaokumbuka, kipindi fulani enzi za Lwandamina Yanga iliwahi kumleta kiungo mkabaji kutoka Cameroon aliyetisha kwa soka lake la nguvu kabla ya dili lake kufa na kusajiliwa Festo Kayembe ambaye hakuwahi kuitumikia timu.


Jamaa huyo ni Fernando Bongyang, ambaye kumbe anafahamiana na Kocha Zahera aliyeshtuka kusikia kiungo huyo alishawahi kupita Yanga kusaka usajili na kuachwa.


Kocha Zahera ametaka kusajiliwa kwa beki wa kati mmoja, beki wa kulia na hata straika wa kati mwingine na kwa upande wa beki wa kati Bongyang anatafutwa tena na mabosi wa Yanga sasa kuja kuanza kazi.


Zahera ametaka kusajiliwa kwa beki, lakini alichokitaka kwa Bongyang ni kufuatia beki huyo kuwa na uwezo wa kucheza pia kama kiungo mkabaji.


Imeelezwa kuwa kocha Zahera anauamini uwezo wa Bongyang na amewaambia mabosi wake kuwa atakapompata mchezaji huyo atakuwa amepiga bao zuri tu.







No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.