KIPINDI CHA USAJILI, MASLAHI YAWE PIA KWA WAZAWA WANAOFANYA VIZURI
NA SALEH ALLY
USAJILI wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara umeshika kasi kwa sasa jambo ambalo linaonyesha kuwa kila timu ilikuwa inasubiri kwa hamu kipindi hiki kifike.
Siyo timu kubwa za Simba na Yanga tu ambazo zinapigana vikumbo kwenye usajili, bali hata zile ambazo awali zilikuwa zinaonekana kuwa hazina presha sana.
Hii inaonyesha kuwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara utakuwa na ushindani wa hali ya juu kwa kuwa kila timu inataka kuziba pengo ambalo lilionekana msimu uliomalizika hivi karibuni.
Mbali na Simba na Yanga, lakini hata timu za Azam, Singida, KMC, Mbao na nyingine nyingi nazo zimekuwa zikipigana vikumbo kwenye usajili huu.
Kwanza ieleweke kuwa dirisha rasmi bado halijafunguliwa, lakini timu zote zinahaha kwa kuwa kila moja inataka kumaliza biashara mapema, jambo ambalo ni zuri kwenye kipindi kama hiki ndiyo maana unaona hata Liverpool tu baada ya kumaliza msimu walimsajili Fabinho, kutoka kwenye kikosi cha Monaco ikiwa hata usajili haujafunguliwa.
Lakini kwa Tanzania, huko nyuma kuna jambo ambalo limekuwa limezoeleka kufanyika kwenye kipindi kama hiki cha usajili.
Imekuwa ikionekana ili mchezaji apewe maslahi mazuri basi lazima awe ametoka nje ya nchi, mchezaji anaweza kutoka Kenya, Uganda, Sudan au hata Ethiopia, akapewa fedha nyingi za usajili kuliko mchezaji anayesajiliwa akitokea Mtibwa Sugar.
Siyo jambo baya kuwapa mishahara mizuri na kuwapa fedha nyingi za usajili, lakini ni kweli huwa wanakuwa na viwango vya juu kuliko wale wanaocheza hapa nchini?
Sidhani kama ni kweli kuna wachezaji hapa nchini wamekuwa wakionyesha kiwango cha juu, wamekuwa wakionyesha nidhamu ya juu sana na wakati mwingine wamekuwa wakijitoa uwanjani kuliko wengine, nafikiri klabu zetu zinatakiwa kuwaangalia hawa.
Mfano mzuri ambao nauona ni wa kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, ambaye naelezwa kuwa alikuwa anagoma kusaini mkataba wa Simba kutokana na maslahi madogo.
Nani anaweza kudiriki kusema kuwa Kichuya hakuwa chachu ya Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika? Nadhani hakuna hata mmoja na ndiyo maana hata viongozi wa Simba hawakusita kumpa mkataba mpya mchezaji huyo mara tu ule wa awali ulipomalizika.
Hili ni jambo zuri na Simba wameonyesha kuwa kuna wakati wa kuwajali wazawa jambo ambalo linaonekana kuwa zuri na picha halisi ya wapi tunakwenda.
Siyo vizuri kuwaona wao hawastahili fedha nyingi kwa kuwa tumezaliwa nao mtaa mmoja, siyo vizuri kuona kuwa hawastahili kupewa nyumba za kuishi ufukweni kwa kuwa tu ni Watanzania.
Nafikiri umefika muda sasa wa viongozi wa klabu kuhakikisha kuwa kama mchezaji ana uwezo, hawana haja ya kuangalia ni raia wa nchi gani, bali wampe maslahi sawa na yule wanayemsajili kutoka Nigeria, Cameroon na hata Ivory Coast.
Itakuwa ajabu leo kama utatazama mkataba halafu ukaona kuwa Kelvin Yondan wa Yanga ambaye alijituma bila kugoma msimu mzima anazidiwa mshahara na mchezaji mwingine kwenye kikosi cha Yanga kwa kuwa tu ametoka nje ya nchi, huku akiwa ndiye kinara wa migomo msimu mzima.
Hakika hii siyo sawa, hata ninapoona mchezaji kama Adam Salamba anatoka Lipuli anaenda Simba, bado natamani kuona mkataba wake ukiwa na maslahi ya kutosha kama mchezaji ambaye atachukuliwa na Simba kwenye Ligi ya Uganda au Rwanda, kwa kuwa ni mchezaji ambaye alifanya kazi kubwa msimu uliopita.
Usajili huu nafikiri ufanyike kisasa zaidi, mameneja wa wachezaji wapunguze tamaa na kukubali kukaa mezani na kuzungumza kuhusu maslahi ya wachezaji wao na siyo wakishakuwa na uhakika wa kupata posho zao wanaharakisha mikataba. Ili wachezaji wajitume ni lazima walipwe vizuri.
Tunaweza kuwa na ligi bora kama tu usajili utafanyika kwa balansi bila kujali ni mchezaji aliyetoka wapi bali awe na uwezo wa hali ya juu
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.