Huyu ndiye John Bocco


TOFAUTI na mwonekano wake, John Bocco ‘Adebayor’ ni hatari asikuambie mtu. Kwa mwonekano jamaa ni kama mzembe fulani hivi, halafu sasa hatishi kwa sababu amejaa haiba ya upole na hata mabeki wasiomjua wanaweza kumchukulia poa.


Hata hivyo, ukifuatilia rekodi zake tangu alipotua katika Ligi Kuu Bara akipanda na Azam msimu wa 2008-2009 mpaka msimu huu wa 2017-2018 unaokuwa wa 10 kwake ndio utajua jamaa huyu ni ‘silent killer’ kwani amewatesa sana mabeki na makipa.


Rekodi za Bocco katika Ligi Kuu Bara zinatisha akiwa ndiye kinara wa mabao mengi kwa sasa akitupia nyavuni mara 98, huku akibeba Kiatu cha Dhahabu mara moja sambamba na mataji mawili ya ligi hiyo aliyobeba akiwa na Azam na Simba.


Mwanaspoti linakudadavulia kwa ufupi rekodi za kusisimua za straika huyu mwenye urefu wa mita 1.9 na kilo 76 aliyeanza kucheza soka Kijitonyama FC, Cosmo kabla ya kudakwa na Azam aliyodumu naye kwa misimu tisa kabla ya kutua Msimbazi.




Msimu wa kwanza


Bocco alianza kuigusa Ligi Kuu msimu wa 2008-2009 baada ya kuibeba Azam katika fainali za Ligi Daraja la Kwanza Kituo cha Dodoma akifunga mabao ya kutosha.


Katika msimu huu ambao Azam iliathiriwa na ushamba wa ligi na kumaliza nafasi ya tisa, Bocco alimaliza akifunga bao moja tu akiitungua Toto Africans.


Katika msimu huu Mkenya Boniface Ambani ndiye aliyekuwa mfungaji bora akitupia mabao 18.




Msimu wa Pili


Katika msimu huu wa 2009-2010, Bocco alishaanza kuizoea ligi kwani alianza kuwahenyesha mabeki na makipa kwa kufunga kadiri alivyopata nafasi. Ndio maana haikuwa ajabu kumaliza msimu akiwa mabao 14 sawa na Mrisho Ngassa wakiwa nyuma ya Mfungaji Bora, Mussa Hassan Mgosi aliyetupia 18.




Msimu wa Tatu


Kwenye msimu huu wa 2010-2011, Bocco aliendelea kutupia kama kawaida yake, lakini hakufikia idadi ya msimu uliopita, hata hivyo, aliwatesa pia mabeki na makipa katika Ligi Kuu.


Bocco alifunga mabao 12 akishika nafasi ya tatu katika msimamo wa wafungaji, akishirikiana na Ngassa aliyeibuka mfungaji bora kipindi hicho wakicheza pamoja Azam FC.




Msimu Mtamu


Huu ndio msimu mtamu kwa Bocco kwani, licha ya kwamba timu yake ya Azam iliendelea kutoa ushindani na kusaka taji la Ligi Kuu, lakini binafsi alitisha zaidi uwanjani kwa kutupia mabao matamu.


Katika msimu huu ulioshuhudia Simba ikibeba lililokuwa taji lake la mwisho kabla ya kufuta mkosi msimu huu wa 2017-2018, Bocco aliibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 19.




Msimu wa Tano


Msimu huu wa 2012-2013 huenda usisahulike kichwani mwa Bocco, kwani majeraha yalimuandama na wakati akichanganya kasi sambamba na Kipre Tchetche ili kuiopa Azam ubingwa, hivyo kujikuta akimaliza na mabao saba na kushindwa kuingia hata kwenye Tatu Bora wa wafungaji wa msimu huu ambao Yanga ilibeba taji.


Hata hivyo, kilichovutia ni straika mwenzake, Kipre ndiye aliyekuwa mfungaji bora na mabao yake 17.




Msimu wa Kibabe


Bocco hawezi kuusahau msimu huu, kwani licha ya kwamba hakutisha kwa mabao, lakini aliiwezesha Azam kubeba taji lake la kwanza la Ligi Kuu.


Mabao yake saba na mengine ya nyota wa timu hiyo yalitosha kuipa matajiri hao taji la msimu wa 2013-2014 na kuweka rekodi ya kipekee ya kukata ufalme wa vigogo uliodumu tangu Mtibwa ilipotwaa taji mara mbili mfululizo 1999 na 2000. Tuzo ya Mfungaji Bora safari hii ilienda kwa Mrundi Amissi Tambwe aliyekuwa Simba akifunga mabao 19.




Msimu Dume


2014-2015 ndio msimu dume kwa Bocco kwani alishinda muda mrefu akijiuguza na kumuacha akimaliza msimu huo na mabao mawili, huku Simon Msuva akibeba kiatu cha dhahabu kwa mabao yake 17.




Arudi kivingine


Msimu wa 2015-16 licha ya Amissi Tambwe akiwa Yanga kuweka rekodi ya mabao 21, lakini Bocco hakuwa nyuma naye alirejesha makali yake na kufunga mabao 12 yaliyoifanya timu yake kumaliza tena nafasi ya pili nyuma ya Yanga iliyobeba ndoo.




Msimu wa Msuva


Katika msimu huu, ulikuwa ni wa Simon Msuva kwani winga huyo wa Yanga ambaye kwa sasa anakipiga Difaa El Jadida ya Morocco alitisha kwa kufumania nyavu akichuana na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting waliomaliza naye sawa kila mmoja akifunga 14.


Hata hivyo, Bocco aliendelea kuboresha rekodi yake ya mabao katika ligi hiyo kwa kufunga mabao 10, manne pungufu na wafungaji bora hao, huku Azam ikimaliza pabaya kwa kushika nafasi ya nne ikiwa ni mara ya kwanza ndani ya misimu mitano kutoka kwenye mbili bora.




Atua Msimbazi


Msimu huu 2017-18 Bocco aliwashtusha mashabiki wa Azam kwa kutua Msimbazi na kuungana na Okwi kuliamsha dude kisawasawa na kuibebesha Simba taji lake la 19 la Ligi Kuu na la kwanza baada ya msoto wa miaka mitano.


Bocco alichangia mabao 14 kati ya 62 yaliyofungwa na Simba na ushirikiano wake na Okwi ulizalisha mabao 34 ikiwa ni zaidi ya nusu ya mabao yote ya timu yake msimu huu, kwani straika Mganda, Okwi alifunga mabao 20 na kuwa kinara wa Ligi Kuu.




Mabao hayo 14 yalimfanya Bocco kutimiza jumla ya mabao 98 katika misimu 10 ya kucheza kwake Ligi Kuu Bara.




Kaseja mteja wa kudumu


Kama hujui katika misimu yote 10 ya kucheza Ligi Kuu kwa Bocco, kipa Juma Kaseja ndiye amekuwa mhanga wake kwa kumtungua mara 10, bao la mwisho likiwa ni katika mechi iliyopigwa mjini Kaitaba msimu huu Simba iliposhinda mabao 2-0.




Usajili wake usipime


Bocco alisajiliwa na Simba baada ya Azam kumtupia virago na Msimbazi walimdaka kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 30 milioni.


Mara alipotua Msimbazi alikabidhiwa jezi namba 22 na baadaye kukabidhiwa unahodha na kuweka rekodi ya kuibebesha Simba taji mapema bila kufungwa. Hata hivyo, rekodi ilichafuliwa na Kagera Sugar iliyoitungua ilipokuwa ikikabidhiwa taji lake na Rais John Magufuli.




Mshahara mnono


Bocco kwa mwaka anavuta Sh 24 milioni kutoka klabu ya Simba kwa maana kila mwezi anachukua Sh 2 milioni, hivyo ni mbali na bonasi na posho nyingine anazopata pale Simba inapopata matokeo mazuri. Pia, ukiondoa mabao yake 14 ya msimu huu katika Ligi Kuu, Bocco ameifungia Simba mabao mengine manne, yakiwamo matatu ya Kombe la Shirikisho Afrika na moja la Kombe la FA.




Awanyoosha watani


Simba na Yanga zilikuwa hazitaki kulisikia jina la Bocco ndio maana zilimgombea alipoachiwa na Azam kabla ya Msimbazi kumnasa.


Kabla ya kutua Msimbazi, Bocco akiwa Azam alizinyoosha timu hizo kongwe nchini, akiitungua Yanga jumla ya mabao 13 na Simba kuifunga mabao 19 na pengine kutua kwake katika timu hiyo kumewapa faraja mashabiki wa Wekundu hao wa Kariakoo ambao walikuwa wakikosa raha kila timu yao ilipokutana na Azam FC. Kwa makali haya, tutarajie nini kwenye msimu unaofuata kwa Bocco.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.