Yanga: Tupo fiti kuwachapa Rayon Sports


Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania Bara, Yanga SC kesho (Jumatano) majira ya saa 1:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, wanatupa karata ya pili ya michezo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.

Yanga ambayo mechi ya kwanza ilianza kwa kuchapwa mabao 4-0 na USM Alger ya Algeria inahitaji ushindi ili kurudisha matumaini kwa mashabiki wake wanaonekana kukosa furaha kutokana na timu yao kuendelea kufanya vibaya kitaifa na kimataifa.

Kuelekea kwenye mtanange huo utakaokuwa LIVE ZBC2, Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub na Kocha Msaidizi, Noel Mwandila wamesema kikosi cha Yanga kiko vizuri tayari kwa mchezo huo kikiwa na matumaini makubwa ya ushindi.

Nadiri amesema wachezaji wanatambua kuwa hautakuwa mchezo rahisi kwao hivyo watapambana kufa na kupona huku wakiongezewa nguvu na wachezaji watatu waliokuwa majeruhi na wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha kesho.

Naye Kocha Mkuu wa Rayon Sports, Ivan Minnaert, amesema timu hiyo imekuja na kikosi kamili na ilikuwa na muda wa kutosha wa kufanya maandalizi ikilinganishwa na mchezo wake wa kwanza ambao ilitoka sare ya bao 1-1 na Gor Mahia ya Kenya.

Leave a Comment