Kessy Awaangukia Mashabiki Yanga


Beki wa kulia wa Yanga Hassani Kessy amewataka mashabiki wa mabingwa hao wa kihistoria wa soka la Tanzania kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa kesho Jumatano kuiunga mkono timu yao itakapokuwa inachuana na Rayon Sports katika mchezo wa pili wa kundi D kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Kessy amesema wamejiandaa kikamilifu kupata matokeo kwenye mchezo huo lakini akasisitiza umuhimu wa mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa 'mzuka' "Unapoingia uwanjani na kukuta mashabiki wengi unapata nguvu ya ziada," amesema Kessy. "Mchezo wa kesho ni muhimu sana kwetu kupata ushindi. Tunahitaji sapoti ya mashabiki." Kessy ni miongoni mwa wachezaji waliofanya mazoezi ya mwisho leo asubuhi kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa moja jioni.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.