YANGA TUMIENI MUDA HUU KUBADILI UPEPO
INAFAHAMIKA wazi kwamba hivi sasa Yanga imekuwa haina matokeo mazuri kwenye michuano inayoshiriki tangu kuondoka kwa aliyekuwa kocha wao mkuu, George Lwandamina raia wa Zambia.
Tangu kuondoka kwa Lwandamina katikati ya mwezi uliopita, Yanga imeshindwa kupata matokeo mazuri katika mechi zake nane za kimashindano ilizocheza mpaka sasa, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Kabla ya hapo, matokeo ya Yanga kwenye mechi zake yalikuwa hivi; Yanga 1-1 Singida, Wolaita Dicha 1-0 Yanga, Simba 1-0 Yanga, Mbeya City 1-1 Yanga, USM Alger 4-0 Yanga, Prisons 2-0 Yanga, Mtibwa 1-0 Yanga na Yanga 0-0 Rayon Sports.
Matokeo hayo si mazuri ikizingatiwa kwamba Yanga ndiyo mwakilishi pekee kimataifa hadi sasa ngazi ya klabu.
Tunafahamu kwamba tangu kuondoka kwa Lwandamina kumeibuka mambo mengi ikiwemo migomo kwa wachezaji wakishinikiza kulipwa maslahi yao jambo ambalo kwa kiasi fulani limechangia matokeo mabaya kwa timu hiyo.
Baada ya mchezo wa juzi wa Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga haitacheza tena mpaka Julai 17, mwaka huu itakapocheza dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, hivyo kipindi hiki cha mwezi mmoja kilichopo hapa kati, lazima kifanyike kitu cha kipekee ili kubadilisha mwelekeo wenu.
Yafanyike maandalizi ya maana, pia kuondoa zile tofauti zenu zilizopo ndani ya klabu ili timu iweze kufanya vizuri. Nadhani muda huu uliopo unatosha kabisa kufanya mabadiliko hayo
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.