Yanga Kukwea "PIPA" Leo


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa Yanga wanatarajiwa kuondoka nchini leo kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa hatua ya Makundi ya kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger nchini Algeria.


Yanga iliyoingia katika hatua makundi ya kombe la Shirikisho baada ya kuwaondoa Welayta Dicha itashuka dimbani Mei 06 kupambana na USM Alger ikiwa ni mchezo wa kwanza wa kundi D.

Baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Simba, Yanga sasa wanaweka nguvu zao zote kwenye mashindano hayo ili kuhakikisha wanazidi kufanya vizuri.

Mkuu wa Kitengo wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga Dismas Ten amesema kuwa kwa sasa nguvu zote wanaelekeza katika mchezo wao wa kombe la Shirikisho kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi yao ya kwanza.

Ten amesema kuwa Yanga wataondoka nchini kupitia Dubai na kisha kuelekea nchini Alger ili kuwahi kufika nchini humo pamoja na kuzoea hali ya hewa.

Yanga kwa sasa inayosimamiwa na kocha msaidizi Shadrack Nswajigwa imekuwa na matokeo sio mazuri toka kuondoka kwa kocha mkuu George Lwandamina kuachana na timu hiyo na michezo minne ambayo imesimamiwa na msaidizi wake ameshindwa kuwapa ushindi.

Ikumbukwe hivi sasa Yanga ndiyo timu pekee inayoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo ya kimataifa baada ya Simba kuondoshwa na Al Masry SC kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ilipangwa kundi moja ‘KUNDI D’ na timu za U.S.M Alger, Rayon Sports na Gor Mahia FC kwenye hatua ya makundi baada ya kuindosha Wolaita Dicha SC ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.