SIMBA MAJARIBUNI SONGEA

Kikosi cha Simba sc


TIMU ya Simba imejikuta majaribuni kuelekea katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Majimaji, utakaochezwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, Ruvuma.
Simba, ambao wameshautwaa ubingwa wa ligi hiyo, wanaweza kuishusha Majimaji iwapo watawafunga wenyeji wao hao katika mchezo huo.
Hivyo, Simba watakuwa na mtihani wa aidha kuwashusha wapinzani wao hao au kuwabakiza Ligi Kuu Bara ili kujenga ‘undugu’ baina yao msimu ujao.
Awali, Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre, alisema pamoja na kutwaa ubingwa, lakini watajitahidi kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo yao yote iliyobaki, ukiwamo wa Jumatatu.
“Pamoja na kuwa mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu, lakini tutahakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu yote iliyobaki,” alisema Pierre. Upande wa Kocha wa Majimaji, Habib Kondo, alisema: “Hakuna mchezaji ambaye atakosekana katika mchezo wetu dhidi ya Simba, kwani tuliujua muda mrefu, tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi tatu na tutazipata tu.”
Majimaji, wenye pointi 24, watalazimika kushinda mchezo huo ili wabaki Ligi Kuu Bara, huku wakiombea Ndanda FC (pointi 26) wapoteze dhidi ya Mwadui. Iwapo Majimaji watashinda Jumatatu na Ndanda nao kupata ushindi, timu hiyo ya Songea itashuka daraja.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.