Simba Kusaka Rekodi Kwa Singida United Leo.



Mabingwa wa ligi kuu ya Vodacom, Simba leo wanashuka kwenye uwanja wa Namfua mkoani Singida kucheza na wenyeji wao Singida United kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom ambao ni wa kukamilisha ratiba tu.

Simba iliyotwaa ubingwa juzi baada ya Yanga kuchapwa mabao 2-0 na Prisons, itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na malengo ya kulinda rekodi yake ya kutopoteza mchezo msimu huu.

Hali ni hiyo hiyo kwa Singida United ambayo imetinga fainali ya kombe la FA, itakuwa nyumbani ikijaribu kulipa kisasi kipigo cha mabao 4-0 ilichopata kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Idara ya Habari ya Klabu ya Simba Haji Manara amesema baada ya mchezo huo Simba itaelekea mkoani Dodoma ambapo keshokutwa Jumatatu itacheza na timu ya 'combine' ya Dododma.

Kabla ya mchezo huo asubuhi Simba itaitikia mwaliko iliyopata kutoka Bungeni.

Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mashabiki wa Simba wamewaalika mabingwa hao wapya Bungeni.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.