Kwasi, Gyan Watajwa Timu Hii VPL


KOCHA msaidizi wa Ndanda FC, Mussa Mbaya, ametoboa siri kuwa waliingia katika mchezo wao dhidi ya Simba wakiwa na lengo la kuwadhibiti Asante Kwasi na Nicolaus Gyan pekee ili wasilete madhara kwenye lango lao.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Ndanda ilifungwa bao 1-0, shujaa akiwa ni Emmanuel Okwi.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mbaya alisema licha ya kufungwa, lengo lao lilifanikiwa kwa asilimia 75 kwani walifanikiwa kudhibiti njia zote zilizokuwa hatari kwao, hasa katika nafasi walizokuwa wakicheza Kwasi na Gyan.

“Simba ukitaka kucheza nao vizuri wazibe pembeni, umeona hata kwenye mchezo wa leo     (juzi) ilibidi wabadilishe aina ya uchezaji. Katika kikosi cha Simba, ukimziba Kwasi na Gyan umefanikiwa,” alisema.

Hata hivyo, kocha huyo alisema wamekubali kipigo walichopewa na Wanamsimbazi hao, wakiamini hawatashuka daraja msimu huu kwani  wataendelea kupambana wabaki Ligi Kuu Bara.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.