Yanga Kurejea Ya Mwaka 2016?.


Yanga inakaribia kabisa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho Barani Afrika, ikihitaji matokeo ya sare au ushindi kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Wolaitta Dicha.

Yanga inaweza kurejea kile ilichokifanya mwaka 2016 nchini Angola kwa kufanikiwa kutinga hatua ya makundi licha ya kuchapwa bao 1-0 na Sagrada Esperanca.

Licha ya figisu nyingi zilizofanywa na Esperanca ikiwa ni pamoja na waamuzi kuwazawadia mkwaju wa penati kwenye dakika za majeruhi, hawakuweza kuizuia Yanga kwani penati hiyo ilipanguliwa na mlinda lango wa wakati huo Deo Munishi 'Dida' na Yanga kushinda kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.

Yanga ilishinda 2-0 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa katika uwanja wa Taifa.

Mapokezi nchini Ethiopia yamekuwa ya kiungwana, leo kikosi cha Yanga kinatarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye dimba la Hawassa kabla ya mchezo huo hapo kesho.

Yanga ina historia ya kutofanya makosa inapopata fursa ya aina hii. 

Aidha, ushindi kwenye mchezo wa kesho utarejesha furaha ya mashabiki ambao baadhi wameonyesha kukata tamaa .

Hata kama Yanga itashindwa kutetea ubingwa wa VPL msimu huu, hakika mafanikio kwenye michuano hiyo yataacha faraja kwa mashabiki wake hasa ikizingatiwa changamoto nyingi zimeikabili Yanga msimu huu.

Milioni 600 si haba!

Ndio! Kwa kufanikiwa kutinga hatua ya makundi tu, Yanga itajihakikishia kitita cha zaidi ya Mil 600, zawadi inayotolewa na CAF kwa timu zote zitakazotinga hatua hiyo.

Zawadi hiyo itaongezeka kadiri ya mafanikio itakayopata timu katika hatua ya makundi, robo fainali, nusu hadi fainali.

Ili kuongeza hamasa kwa wachezaji, uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa kama wachezaji watafanikisha azma ya kutinga makundi, sehemu ya pesa hiyo itakuwa yao.

Hii itakuwa shukrani kwa wachezaji kutokana na kazi kubwa waliyoifanya licha ya changamoto lukuki zinazowakabili msimu huu.

Pia wachezaji watapata faida zaidi ya kuonekana Kimataifa iwapo timu itatinga Makundi. 

Michuano ya CAF hatua ya makundi inarushwa mubashara na runinga nyingi ndani na nje ya Afrika.

Hatua hiyo itahusisha makundi manne ya timu nne nne. Kila timu itacheza michezo sita, mitatu nyumbani na mitatu ugenini.

Mshindi wa kwanza na wa pili kutoka kila kundi watatinga hatua ya robo fainali itakayochezwa kwa mtoano mechi mbili za nyumbani na ugenini.

Hivyo hivyo itakuwa hatua ya nusu fainali na fainali inayotarajiwa kupigwa mwishoni mwa mwezi Novemba 2018.

Yanga itakuwa imefanikiwa zaidi msimu huu kama itafanya vizuri kwenye michuano hii.

No comments:

Note: only a member of this blog may post a comment.