VPL: Raundi ya 23 kuanza ijumaa
Raundi ya 23 ya ligi kuu soka Tanzania Bara inatarajiwa kuanza ijumaa kwa michezo miwili ambayo itafanyika katika viwanja vya miji ya Singida na Mwanza.
Mabingwa wa zamani kwa mara mbili mfulululizo mwaka 1999 na 2000 Mtibwa Sugar ya kutoka mji kasoro bahari, watakuwa na kibarua kizito watakapocheza na walima alizet timu ya soka ya Singida United.
Mtanange huo mkali na wa aina yake utafanyika kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida ambapo Mtibwa ambayo ilianza vyema msimu huu watakuwa wakitafuta ushindi wa kwanza toka kuanza kwa mzunguko wa pili.
Mbao vs Lipuli
Katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza, Wanapaluhengo timu ya soka ya Lipuli FC itacheza na wenyeji Mbao FC ambao wapo katika mapambano makali ya kukwepa kushuka daraja.
Mpaka sasa Mbao FC wamepoteza michezo mitano kati ya michezo saba ya mzunguko wa pili waliyokwishakucheza, wakishinda mchezo mmoja pekee matokeo yanayowafanya kuwa katika nafasi ya 14 na alama zao 19.
Kwa upande wa Lipuli wao wamepoteza mchezo miwili kati ya hiyo michezo saba wakitoka sare michezo miwili na kushinda michezo mitatu, na hivyo kufikisha alama 27 zinazowafanya kuwa katika nafasi ya saba.
Jumamosi April 7
Mechi nyingine za Raundi ya 23 ni pamoja na Mwadui FC kucheza na Majimaji FC siku ya Jumamosi Aprili 7, 2018 katika uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.
MCC vs Azam
Jumapili Aprili 8,2018 Mbeya City watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa kumbukumbu ya sokoine jijini Mbeya kuwakaribisha mabingwa mara moja wa taji hilo, Azam FC.
Nao Wapiga debe wa Shinyanga timu ya soka ya Stand United wao watakuwa nyumbani katika dimba la CCM Kambarage kucheza na Njombe Mji, huku Ndanda FC wakicheza na Kagera Sugar katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mechi ya mwisho kwa wikiend hii za raundi ya 23 itakuwa kati ya Wafunga buti Ruvu Shooting kucheza na Wajelajela Tanzania Prisons katika uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.
Vinara
Mpaka sasa Simba ndio vinara wakiwa na alama 49 wakifuatiwa na Yanga wenye alama 46, na wa tatu ni Azam wenye alama 44 huku mkiani wakikaa Njombe Mji, Majimaji na Mbao FC.
Aidha msimu huu zitashuka timu mbili badala ya tatu ili kupisha timu sita kutoka ligi daraja la kwanza kufanya msimu ujao kuwa na timu 20 zitakazowania nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Join us on WHATSAPP Usipitwe Na Breaking News Za Soka: Jiunge nasi kupitia Facebook, Bofya LIKE Button...
No comments:
Note: only a member of this blog may post a comment.